YEMEN-Mapigano-Siasa-Usalama

Yemen : mabomu yaendelea kurushwa Sanaa

Mapigano yameendelea kurindima nchini Yemen kati ya vikosi vya rais Abd Rabbo Hadi Mansour na wanamgambo wa Kishia kutoka jamii ya Houthi katika mji wa Aden wenye Bandari kubwa, kusini mwa nchi hiyo.

Raia wakiendelea kuukimbia mji mkuu wa Yemen, Sanaa, Machi 29 mwaka 2015.
Raia wakiendelea kuukimbia mji mkuu wa Yemen, Sanaa, Machi 29 mwaka 2015. AFP PHOTO / MOHAMMED HUWAIS
Matangazo ya kibiashara

Mapigano kati ya wapiganaji kutoka jamii ya Wasuni na waasi wa Kishia kutoka jamii ya Houthi yamesababisha vifo vya zaidi ya watu arobaini.

Hata hivyo muungano wa nchi kumi za kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia umeendelea na mashambulizi ya angani usiku wa kuamkia Jumapili mwishoni mwa juma hili. Hali ya wasiwasi imeendelea kutanda katika mji wa Sanaa na miji mingine mikubwa inayoendelea kushuhudia mashambulizi ya angani.

Kwa sasa mashambulizi hayo yanaendeshwa karibu na eneo la visima vya mafuta, kusini mwa Yemen. Jumapili juma hili, mapigano yaliripotiwa kati ya wapiganaji kutoka jamii ya Wasuni na waasi wa Kishia kutoka jamii ya Houthi na washirika wao, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu arobaini, kwa mujibu wa taarifa za shirika moja la habari nchini Yemen.

Kwa upande wake, muungano unaoendeshwa na Saudi Arabia umeendelea na mashambulizi ya angani. Ndege za kivita zimeendesha mashambulizi ya angani katika uwanja wa ndege wa mji wa Sanaa.

Kwa siku ya tatu ya mashambulizi hayo, raia wameanza kuukimbia mji wa Sanaa, wakati ambapo zaidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, balozi na makampuni ya kigeni waliondoka nchini Yemen, huku manuari ya jeshi la Saudi Arabia ikisaidia kuwasafirisha wanadiplomasia kutoka katika mji wa Aden, kusini mwa nchi hiyo.