URUSI-UCHUMI-SIASA

Putin aendesha mjadala na raia wake

Rais wa Urusi Vladimir Putin amelihutubia taifa Alhamisi wiki hii na baadae amehojiwa na rai wake kuhusu masuala nyeti yanayoikabili nchi hiyo wakati huu, hususan katika sekta ya uchumi sera za nje na kadhalika.

Rais Vladimir Putin akihojiwa na raia wake, katika kipindi kilichopeperushwa hewani moja kwa moja.
Rais Vladimir Putin akihojiwa na raia wake, katika kipindi kilichopeperushwa hewani moja kwa moja. Reuters
Matangazo ya kibiashara

Rais Putin amelihutubia taifa kwa muda wa saa moja, ambapo aligusia hasa suala la uchumi, ambao unaoneka kudorora nchini humo. Vladimir Putin amejaribu kuwaweka sawa raia wake, wakati ambapo mapato ya raia wa Urusi yameshuka tangu mwanzoni mwa mwaka huu kufuatia kupoteza thamani kwa pesa za Rouble.

Rouble imeendelea kupoteza thamani tangu majuma mawili yaliyopita. Mapema asubuhi Alhamisi Aprili 16, Rouble 50 imekua ikiuzwa Dola moja. Rais Putin amethibitisha kwamba pesa ya Urusi imepoteza thamani. Hata hivyo amewapa matumaini raia wake kwamba atahakikisha hali hiyo imepatiwa ufumbuzi.

“ Tutaondokana na hali hii haraka iwezekanavyo, katika kipindi cha miaka miwili”, amesema rais Putin.

Hata hivyo Putin amesema hatasubiri mpaka vikwazo ambavyo Urusi iliyowekewa viondolewe, kwani amesema vikwazo hivyo ni vya kisiasa, ambavyo haviambatani na suala la Ukriane

Putin ametangaza pia kwamba hakuna umuhimu wowote kwa Ufaransa kukataa kuikabidhi meli za kivita iliyonunua. Putin amekanusha kwamba urusi ina nia ya kurejesha maeneo iliyoyapoteza baada ya kujitenga, huku akitambua kwamba kuweka utawala wa Kisovietiki barani Ulaya baada ya mwaka 1945 sio kitu kizuri.