ICC-URUSI-GERGIA-SHERIA

ICC yaanzisha uchunguzi kuhusu vita vya Georgia na Russia mwaka 2008

Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC Fatou Bensouda Reuters

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Jumatano hii, imemruhusu mwendesha mashitaka kuchunguza vita vilivyotokea mwezi Agosti 2008 kati ya Georgia na Urusi kwa llengo la udhibiti wa eneo la Ossetia Kusini, Mahakama imetangaza.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama hii inatoa nafasi kwa uchunguzi wake wa kwanza kuhusu madai ya uhalifu uliofanywa na majeshi ya Urusi, na uchunguzi wake wa kwanza kuhusu mgogoro usiokuwa wa Kiafrika.

Mwendesha mashitaka Fatou Bensouda aliomba ruhusa mwezi Oktoba kuanzisha uchunguzi, akidai kuwa ana ushahidi kwamba uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita ulitekelezwa katika vita hivyo.

"Mahakama imemtendea haki mwendesha mashitaka kuchunguza hali iliyojiri nchini Georgia", ICC imesema katika taarifa yake.

Majaji wamebaini kwamba "kuna ukweli katika madai ya mwendesha mashitaka" kwamba uhalifu ikiwemo mauaji, mateso, kuwaondoa raia kwa nguvu na uporaji vilifanywa kati ya Julai 1 na Oktoba 10, 2008.

Mapigano kati ya Urusi na Georgia yalidumu siku 5 mwezi Agosti 2008 katika vita vilivyoibuka, na kumalizika kwa ushindi wa Urusi, kwa udhibiti wa eneo la Ossetia Kusini, eneo la Georgia lililojitenga na kuungwa mkono na Urusi

Kremlin baadae ilitambua uhuru wa eneo hili.

Mgogoro huo uligharimu maisha ya watu wengi na zaidi ya watu 120,000 walikimbia makazi yao, kulingana na ripoti ya mwezi Agosti 2008 ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashitaka, idadi ya watu wenye asili ya Georgia katika eneo hilo la Ossetia Kusini "ilipungua angalau 75%."