UKRAINE-URUSI-NATO

NATO yaitolea wito Urusi kuondoa vikosi vyake Ukraine

Katibu mkuu wa Nato Jens Stoltenberg (kulia) na Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Stepan Poltorak wakati wa mkutano kwenye makao makuu ya Nato Brussels Juni 15, 2016.
Katibu mkuu wa Nato Jens Stoltenberg (kulia) na Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Stepan Poltorak wakati wa mkutano kwenye makao makuu ya Nato Brussels Juni 15, 2016. JOHN THYS/AFP

Katibu mkuu wa Umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi (NATO) Jens Stoltenberg ametoa wito kwa mara nyingine tena leo Jumatano kwa Urusi kusitisha msaada wake kwa waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Matangazo ya kibiashara

Bw Stoltenberg ameitaka pia Urusi "kuondoa vikosi vyake pamoja na vifaa vya kijeshi" nchini humo, ikiwa ni pamoja na katika eneo la Crimea.

"Urusi inapaswa kusitisha msaada wake kwa wanamgambo (waasi wanaotaka kujitenga) na kuondoa vikosi vyake na vifaa vya kijeshi katika ardhi ya Ukraine,"

Stoltenberg ametangaza katika siku ya pili na ya mwisho ya mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Umoja huo mjini Brussels. Mawaziri hao wamempokea leo Jumanne asubuhi mwenzao wa Ukraine, Stepan Poltorak.

Kiongozi huyo wa NATO amesema kuwa wakuu wa nchi na serikali za nchi 28 wanachama wa NATO wataonyesha "uungwaji wao mkono (...) kwa uhuru na mipaka ya Ukraine" kwa kumpokea Rais Petro Poroshenko wakati wa mkutano wao ujao katika mji wa Warsaw tarehe 8 na 9 Julai.

Moscow imeendelea kukanusha kutoshiriki moja kwa moja bega kwa bega na waasi katika vita hivyo ambavyo vimegharimu maisha ya zaidi ya watu 9,300 tangu majira ya joto 2014.

Bw Stoltenberg ameelezea masikitiko yake kwamba, katika uwanja wa vita mashariki mwa Ukraine, "ukiukaji wa usitishwaji mapigano unaendelea siku baada ya siku na waangalizi wa OSCE (Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya) wanaendelea kuzuiliwa katika kazi zao" kwa kusimamia utekelezaji wa mkataba wa usitishwaji wa mapigano.

"Mikataba ya Minsk, inayotoa nafasi ya kumaliza mgogoro, "ni njia pekee ya kupata suluhisho la kudumu nchini Ukraine. Ni kwa pande zote kuharakia kuweka mbele utekelezaji huo", Katibu mkuu wa NATO amesema.