UGAIDI

Bangladesh yatangaza siku mbili za maombolezo baada ya shambulizi la kigaidi

Wanajeshi wakiwa nje ya Hoteli ya Holey Artisan baada ya shambulizi la kigaidi IJumaa usiku
Wanajeshi wakiwa nje ya Hoteli ya Holey Artisan baada ya shambulizi la kigaidi IJumaa usiku Reuters/路透社

Serikali ya Bangladesh imetangaza siku mbili za maombolezo baada ya watu 20 wengi wao raia wa kigeni kuuliwa na wanajihadi wa Kiislamu.

Matangazo ya kibiashara

Akilihutubia taifa siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu Sheikh Hasina amelaani mauaji hayo na kuwataka wanajihadi hao kuacha kutekeleza mauaji dhidi ya watu wasiokuwa na hatia kwa kisingizio cha kupigania dini ya Kiislamu ambayo amesema ni dini ya amani.

Jeshi nchini humo linasema, wanajihadi hao walivamia mkahawa mmoja jijini Dhaka Ijumaa usiku na kuwateka wateja waliokuwemo na baadaye kuwauawa kwa kuwapiga risasi.

Jeshi lilifanikiwa kumaliza operesheni kujaribu kuwaokoa mateka hao baada ya saa 12 na kuwauawa wanajihadi sita huku mmoja akikamatwa na wateka wengine zaidi ya 10 wakiokolewa.

Kundi la Islamic State limekiri kutekeleza shambulizi hili.

Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi amesema raia wa nchi yake ni miongoni mwa watu waliuliwa.

Ripoti kutoka Italia zinasema raia wake 10 ni miongoni mwa watu hao walipoteza maisha.

Serikali ya Japan inasema raia wake pia ni miongoni mwa watu waliouawa.