CHINA

Wabunge nchini China waidhinisha mkataba wa Kimataifa wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa

Kiwanda kinachotoa gesi yenye sumu nchini China
Kiwanda kinachotoa gesi yenye sumu nchini China businessinsider.com

Bunge nchini China limeidhinisha makubaliano ya mkataba wa Kimataifa wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa yenye lengo la kupunguza joto duniani.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imethibitishwa na Shirika la Habari nchini humo la Xinhua.

Awali, ilikuwa imeripotiwa kuwa nchi hiyo inayoongoza kutoa gesi yenye sumu kutokana na utajiri wake wa viwanda, ingetangaza hatua yake ya kuanza kuridhia mkataba huo  pamoja na Marekani pembezoni mwa mkutano wa kiviwanda wa G20 unaofanyika mwishoni mwa wiki hii nchini humo.

Hii imeoneka kuwa hatua kubwa katika kufanikisha makubaliano hayo na kupambana na mabadiliko ya hewa duniani baada ya mkataba huo kuafikiwa mwezi Desemba mwaka uliopita nchini Ufaransa.

Wachambuzi wa maswala ya hali ya hewa na Mazingira wanasema  China imeonesha mfano bora na ikiwa Marekani ambayo ni ya pili kwa kuzalisha gesi hiyo yenye sumu itaidhinisha mkataba huo, basi kiwango cha kudhibiti uzalishaji wa gesi yenye sumu itafikia asilimia 40.

Mataifa mengine zaidi ya 20 ambayo tayari yamekubali kuanza kutekeleza makuabiliano hayo, uzalishaji wake wa  gesi yenye sumu haifiki hata asilimia 1.