SAMSUNG NOTE 7

Kampuni ya Samsung matatani tena, yasitisha uzalishaji wa simu aina ya Galaxy Note 7

Simu aina ya Galaxy Note 7 ambazo zimegizwa kurejeshwa kiwandani kutokana na matatizo ya kuwaka moto.
Simu aina ya Galaxy Note 7 ambazo zimegizwa kurejeshwa kiwandani kutokana na matatizo ya kuwaka moto. REUTERS/Kim Hong-Ji

Kampuni ya utengenezaji simu ya Samsung, imejikuta ikipata pigo jingine kufuatia kuagiza kurejeshwa kiwandani kwa simu zake aina ya Galaxy Note 7, ikikiri kuwa inafanyia marekebisho simu hizo baada ya wasambazaji wakubwa kusitisha utoaji wa simu mpya kutokana na kasoro za kiusalama zilizojitokeza tena.

Matangazo ya kibiashara

Kampuni hiyo ya Korea Kusini inaendelea kukabiliwa na changamoto ya kufanyia marekebisho simu zake baada ya September 2 mwaka huu kuagiza kurejeshwa kiwandani kwa simu zake milioni 2 na laki 5 aina ya Note 7 kutokana na malalamiko ya wateja wake kuwa betri zake zinalipuka wakati zikichajiwa.

Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, kumeibuka taarifa kuwa hata simu zilizokuwa zimerejeshwa sokoni kama mbadala pia zinashika moto, hali iliyofanya kampuni ya uuzaji simu ya kimarekani ya AT and T na ile ya Kijerumani ya T-Mobile kutangaza kusitisha usambazaji wa simu zilizofanyiwa marekebisho wakitaka uchunguzi zaidi.

Tangazo la makampuni haya makubwa Marekani na Ujerumani, limesababisha kushuka kwa thamani ya hisa za kampuni ya Samsung kwenye soko la dunia, ambapo zimeshuka kwa zaidi ya asilimia 4.

Taarifa za kimasoko zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya Korea Kusini, zinasema kuwa kampuni hiyo pia, imetangaza kusitisha kabisa uzalishaji wa simu aina ya Note 7 baada ya kuwa na mazungumzo na mamlaka ya watumiaji huduma kuhusu usalama wa simu hizo kutoka Korea, Marekani na China.

Kampuni ya Samsung inasema kuwa hatua ilizochukua ni kwaajili ya kuwahakikishia usalama wa simu zake wateja wake na kuruhusu uchunguzi zaidi kufanyika kuhusu tatizo lililojitokeza katibu kwenye simu zake zote zilizouzwa hivi karibuni.