UKRAINE-USALAMA

Ukraine: Polisi wawafyatulia risasi wenzao, watano wafariki

Nchini Ukraine, polisi watano wameuawa katika urushianaji risasi na polisi wengine, ambao walihisi kuwa ni kundi la majambazi. Tukio hili la kustaajabisha lilitokea usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili hii Desemba 4, karibu na mji wa Kiev.

Polisi yachunguza tukio la uhalifu katika mji wa Kniazitchi karibu na mji wa Kiev Jumapili hii Desemba 4, 2016.
Polisi yachunguza tukio la uhalifu katika mji wa Kniazitchi karibu na mji wa Kiev Jumapili hii Desemba 4, 2016. SERGEI SUPINSKY / AFP
Matangazo ya kibiashara

Tukio hili lilianza na kuingiliwa kati kwa vikosi maalum vya Ukraine. Walikua katika hatua ya kulitokomeza "kundi hatari la majambazi" wakati kulitokea kelele za wezi. Kikosi cha ulinzi wa taifa na polisi walitumwa eneo la tukio. Wakati huo waliwakamata askari wawili wa kikosi maalum waliokua wakijipanga kukabiliana na kundi hilo, wakiamini kwamba wamewakamata majambazi.

Askari wengine walifikiria kwa upande mwengine kwamba wahalifu wamewateka wenzao. Papo hapo risasi zilirushwa dhidi ya polisi.

Baada ya tukio hilo, maafisa wawili wa kikosi cha ulinzi wa taifa, polisi wawili na askari mmoja wa vikosi maalum vya Ukraine waliuawa.

Wakati huo huo, majambazi walitimka wakielekea mjini Kiev. Lakini walikamatwa haraka. Ofisi ya mashitaka imetangaza kwamba iko mbioni kuanzisha uchunguzi. Rais wa Ukraine kwa upande wake, ameomba wahusika waadhibiwe kwa tukio hili aliloliita "janga la kusikitisha".