URUSI-AJALI

Rais Putin ataka uchunguzi ufanyike kuhusu ajali ya ndege

Ndege aina ya Tupolev 154 kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi wa Chkalovsky mjini Moscow (picha ya zamani).
Ndege aina ya Tupolev 154 kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi wa Chkalovsky mjini Moscow (picha ya zamani). REUTERS/Dmitry Petrochenko

Rais Putin ameagiza uchunguzi ufanywe kuhusu ndege ya jeshi la Urusi, iliyoanguka katika Bahari ya Black Sea, punde baada ya kuondoka Sochi, ikielekea Syria.

Matangazo ya kibiashara

Ndege ya jeshi la Urusi, iliyobeba watu zaidi ya 90, imeanguka katika bahari ya Black Sea , punde baada ya kuondoka Sochi, ikielekea Syria.

Wizara ya Ulinzi imesema hakuna mtu aliyenusurika.

Shughuli za zakuitafuta ndege hiyo zimeendelea katika bahari ya Black Sea. Na tayari mabaki ya ndege yamepatikana kilomita moja na nusu kutoka mwambao.

Mamlaka ya usafiri wa anga nchini Urusi imesema kuwa hapakuwa na ishara ya matatizo, na rubani alisikika ametulia, hadi ndege ilipotoweka.

Abiria wengi walikuwa kutoka kikundi cha bendi ya muziki cha jeshi kwa jina Alexandrov Ensemble. Wanamuziki hao walitarajiwa kufanya tamasha ya mwaka mpya katika kambi ya Urusi mjini Latakia, Syria.

Inaarifiwa kuwa ndege hiyo ilipotea katika mitambo ya Rada, muda mfupi baada ya kupaa angani, kutoka kwenye uwanja wa hoteli moja iliyoko maeneo ya Black Sea katika mji wa Sochi.