URUSI-MAREKANI-USHIRIKIANO

Urusi mbioni kulipiza kisasi kwa Marekani

Rais Vladimir Putin akanusha madai ya utawala wa Barack Obama kuwa aliingilia masuala ya Uchaguzi wa Marekani kwa kumsaidia Donald Trump..
Rais Vladimir Putin akanusha madai ya utawala wa Barack Obama kuwa aliingilia masuala ya Uchaguzi wa Marekani kwa kumsaidia Donald Trump.. REUTERS/Sergei Karpukhin

Urusi imesema italipiza kisasi hatua ya Marekani kuwafukuza wanadiplomasia wake 35 kwa madai kuwa iliingilia Uchaguzi wa urais nchini Marekani kwa kudukua mitandao yake.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa rais Vladimir Putin amesema majibu ya Urusi, yataifanya Marekani kutatizika.

Hata hivyo, Urusi imesema kuwa hatua hii huenda ikachukuliwa baada ya rais mteule Donald Trump kuapishwa baadaye mwezi Januari mwaka ujao.

Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani imewapa wanadiplomasia hao saa 72 kuondoka na familia zao nchini humo.

Pamoja na wanadiplomasia hao wanaofanya kazi kwenye Ubalozi wa Washington DC na San Francisco, Marekani imetanagza vikwazo dhidi ya Mashirika tisa ya Urusi nchini humo zikiwemo kufungwa kwa taasisi mbili za kiitelijensia za GRU na FSB.

Wiki kadhaa zilizopita, rais Barrack Obama aliahidi kuiwekea vikwazo Urusi kwa madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani na kumsaidia Trump kushinda, madai ambayo Urusi imekanusha.

Trump amekanusha kusaidiwa na Urusi kushinda uchaguzi na kuwataka raia wa nchi hiyo kusonga mbele na maisha yao baada ya Uchaguzi.