KOREA KUSINI

Korea Kusini: Mahakama ya katiba kuanza vikao vya kesi dhidi ya rais Park

Mahakama ya katiba nchini Korea Kusini, imefanya kikao chake cha kwanza katika kesi ya kuamua ikiwa ithibitishe kuondolewa madarakani kwa rais Park Geun-Hye au la, kikao ambacho hata hivyo kiongozi huyo hakuudhuria. 

Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye.
Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye. ©Yonhap/ via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Kikao hichi, kilichofuatiwa na vikao vingine vitatu mwezi uliopita, kilidumu kwa dakika 9 pekee kabla ya majaji wanasikiliza kesi hiyo kuiahirisha hadi Alhamisi ya wiki hii.

Mahakama hii pia, juma lililopita ilitoa uamuzi ikisema rais Park hakuwa anahitajika kuhudhiria vikao vya kesi yake wala kuhojiwa.

"Tutafanya kadiri ya uwezo wetu, kutenda haki na kupitia vizuri kesi hii," alisema Park Han-Chul, jaji kiongozi kwenye kesi hiyo na anayeongoza jopo la majaji 9 kwenye kesi hiyo.

Bila kujali ikiwa rais Park atahudhuria vikao vya kesi yake vitakapoanza, kesi hiyo itaendelea kama ilivyopangwa siku ya Alhamisi, huku mawakili wake wakisema uwezekano ni mdogo sana kwa mteja wao kuhudhuria.

Bunge la nchi hiyo lilipiga kura Desemba 9 kumuondoa madarakani rais Park kufuatia tuhuma za rushwa ambazo zilisababisha maelfu ya raia kuandamana kushinikiza achukuliwe hatua.

Park alivuliwa madaraka ya kutekeleza majukumu yake na kwa wakati huu nchi hiyo inaongozwa na waziri mkuu Hwang Kyo-Ahn.