KOREA KUSINI

Korea Kusini: Mahakama yaidhinisha kuondolewa madarakani kwa rais Park Geun-hye

Majaji wa mahakama ya katiba nchini Korea Kusini, wakati walipotoa hukumu kuhusu kumuondoa madarakani Park Geun-hye. Machi 10, 2017.
Majaji wa mahakama ya katiba nchini Korea Kusini, wakati walipotoa hukumu kuhusu kumuondoa madarakani Park Geun-hye. Machi 10, 2017. REUTERS/Kim Min-hee/Pool

Mahakama ya katiba nchinik Korea Kusini hatimaye imekubali kuondolewa madarakani kwa rais aliyekuwa amesimamishwa, Park Geun-hye, ambaye anakuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, kulazimishwa kuondoka madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Majaji wa mahakama ya katiba kwa kauli moja wameidhinisha uamuzi wa bunge la nchi hiyo kumuondoa madarakani rais Geun-hye, kutokana na ushiriki wake katika masuala ya rushwa yakimuhusisha rafiki yake wa karibu Choi Soon-sil.

Kwa uamuzi huu sasa, inamaana kuwa anapoteza kinga zote za urais alizokuwa nazo na huenda akakabiliwa na mashtaka.

Wafuasi wa rais Park Geun-hye ambaye sasa amevuliwa madaraka yake rasmi kutokana na uamuzi wa mahakama ya katiba.
Wafuasi wa rais Park Geun-hye ambaye sasa amevuliwa madaraka yake rasmi kutokana na uamuzi wa mahakama ya katiba. Lim Se-young/Yonhap

Kumeshuhudiwa makabiliano ya polisi na wafuasi wa Park nje ya mahakama ya katiba, ambapo wafuasi wake wanapinga kiongozi wao kuondolewa madarakani na wanapinga uamuzi huu wa mahakama.

Shirika la habari la Korea Kusini Yonhap, limeripoti kuwa watu wawili wamekufa, akiwemo mzee mmoja ambaye alianguka kutoka kwenye gari la polisi, hata hivyo taarifa zaidi bado zinaendelea kuibuka.

Uamuzi huu wa mahakama ni hitimisha la miezi kadhaa ya maandamano yaliyoanza mwaka jana dhidi ya utawala wa rais Park Geun-hye.

Maandamano yaliyokuwa yakimpinga rais Park Geun-hye.
Maandamano yaliyokuwa yakimpinga rais Park Geun-hye. REUTERS/Kim Hong-Ji

Park alisimamishwa kazi za urais toka mwezi Desemba mwaka jana baada ya bunge kupiga kura kutaka aondoke marakani, huku waziri mkuu akikaimu majukumu yake.

Kwa uamuzi huu wa mahakama una maanisha kuwa nchik ya Korea Kusini itahitajika kuchagua rais mwingine mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu.

Kwa wakati huu rafiki wa Park, Choi ameshashtakiwa kwa makosa ya kutoa hongo na kwamba alitoa shinikizo kwa makampuni makubwa kutoa fedha ili yapate msamaha wa Serikali, rais Park amekuwa akituhumiwa kujihusisha kwenye kashfa hii.