INDIA-NIGERIA

Polisi India yawashikilia watu 5 kwa tuhuma za kuwashambulia wa Afrika

Mmoja ya waandamanaji akiwa amebeba bango kukashifu vitendo vya ubaguzi.
Mmoja ya waandamanaji akiwa amebeba bango kukashifu vitendo vya ubaguzi. REUTERS/Neil Hall

Polisi nchini India imewakamata wanaume wa 5 baada ya mamia ya wakazi wa mji mmoja wa kaskazini mwa nchi hiyo kumshambulia raia mmoja wa Afrika kwa fimbo na vyuma kufuatia kifo cha mtoto mmoja kinachodaiwa kutokana na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

Matangazo ya kibiashara

Mamia ya watu wamajeruhiwa kwenye vurugu hizo kwenye mji wa Greater Noida, eneo ambalo linaishi raia wengi kutoka barani Afrika ambao wanasoma nchini humo.

Kulikuwa na uvumi kuwa wa Afrika ndio waliohusika na kifo cha kijana raia wa India na maneno ya kibaguzi yalisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo Polisi wanasema ni wazi ujumbe mwingi ulichochewa kibaguzi.

Afisa wa Polisi kwenye mji huo Sujata Singh amesema kuwa washambuliaji wa tano wamekamatwa na wengine wa nne wamekimbia na wanatafutwa na vyombo vya usalama.

Polisi kwenye mji huo wanasema watu zaidi ya 300 walihusika kwenye vurugu hizo.

Wizara ya mambo ya nje ya India imekashifu vurugu hizo, ambapo imetoa hakikisho kwa balozi wa Nigeria ambaye raia wake nditye aliyeshambuliwa kuwa Serikali imechukua hatua stahiki kuwalinda raia wa kigeni.

Raia wengi wa Nigeria ndio walikuwa wamelengwa kwenye shambulio hilo ambapo vurugu zilizuka baada ya Polisi kuwaachia vijana wa tano wa Nigeria waliokuwa wakituhumiwa kuhusiana na kifo cha kijana huyo.

“Serikali imejidhatiti kuhakikisha usalama na ulinzi wa raia wote wa kigeni nchini India. Watu kutoka Afrika wakiwemo wanafunzi na vijana bado wanasalia kuwa watu wa thamani sana kwao,” ilisema taarifa ya wizara.

Afisa wa Polisi amesema kuwa wananchi walikuwa wamekusanyika kwenye eneo moja kwaajili ya kutoa shukrani na heshima kutokana na kifo cha kijana wao lakini vurugu ziliibuka baada ya watu waliokuwepo kubaini kundi la raia kadhaa wa Nigeria.

Televisheni moja nchini India imeonesha wananchi wakishambulia gari moja kwa fimbo huku wengine wakiwashambulia wateja kwenye duka moja.