KOREA KUSINI

Rais wa zamani wa Korea Kusini Park Geun-Hye akamatwa

Aliyekuwa rais wa Korea Kusini Park Geun-hye akiwa mahakamano Alhamisi ya Machi 30, 2017 kabla ya kukamatwa kwake.
Aliyekuwa rais wa Korea Kusini Park Geun-hye akiwa mahakamano Alhamisi ya Machi 30, 2017 kabla ya kukamatwa kwake. REUTERS/Ahn Young-joon/Pool

Rais wa Korea Kusini aliyeondolewa madarakani kwa tuhuma za rushwa, Park Geun-hye amekamatwa na anazuiliwa na polisi baada ya mahakama ya mjin Seul kuridhia kutoa hati ya kukamatwa kwake kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Matangazo ya kibiashara

Geun-hye alisafirishwa hadi kusini mwa mji wa Seul ambako anazuiliwa kwenye jela moja akisubiri kusikilizwa kwakesi yake.

Anatuhumiwa kwa kukubali rafiki yake wa karibu Choi Soon-sil kujipatia fedha kutoka kwenye makampuni makubwa nchini humo ikiwemo Samsung kwa lengo la kufadhiliwa kisiasa.

Park mwenye ambaye aliondolewa madarakani mapema mwezi huu, amekana kutenda kosa lolote.

Shirika la habara nchini humo Yonhap linaripoti kuwa Park Geun-hye anakuwa rais wa tatu kukatwa kwa makosa ya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.

Mahakama ya Seul ilitoa hati ya kukamatwa kwake na kuzuiliwa kwa muda wakati uchunguzi dhidi yake ukiendelea, anachunguzwa kwa tuhuma za rushwa, matumizi mabaya ya ofisi na kuvujisha siri muhimu za Serikali.

Kukamatwa kwake kumekuja baada ya karibu saa 9 za mahojiano mahakamani.
“Inaelezeka na ni muhimu kumkamata Park hasa kutokana na kuwa mashtaka dhidi yake yanaelezeka na kuna uwezekano wa ushahidi kuharibiwa akisalia nje,” alisema jaji aliyetoa uamuzi wa kukamatwa kwake.

Matangazo mubashara ya televisheni za nchi hiyo, yamemuonesha Park akiwa amechukuliwa kwenye gari maalumu kupelekwa kwenye kituo ambacho atakuwa anazuiliwa huko.

Wafuasi wake walijitokeza nje ya mahakama hiyo wakiwa na bendera ya taifa na wakitaka aachiwe huru.

Park anaweza kuzuiliwa kwa zaidi ya siku 20 kabla ya kushtakiwa rasmi, ikiwa atakutwa na hatia ya makosa yanayomkabili huenda akahukumiwa kifungo cha miaka 10 jela.