KOREA KASKAZINI-MAREKANI-UN

Korea Kaskazini yafanya jaribio jingine yakaidi onyo la Marekani

Watu wakitazama kwenye TV jaribio la kombora la masafa marefu la Korea Kaskazini.
Watu wakitazama kwenye TV jaribio la kombora la masafa marefu la Korea Kaskazini. REUTERS/Kim Hong-Ji

Nchi ya Korea Kaskazini imefanya jaribio jingine la kombora la masafa marefu Jumamosi hii katika kile kinachoonekana ni kukaidi kitisho cha Serikali ya Marekani kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya utawala wa Pyongyang.

Matangazo ya kibiashara

Jaribio hili ambalo Korea Kusini imesema halikufanikiwa, limekuja ikiwa ni saa chache tu zimepita toka waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alionye baraza la usalama kwa kile alichosema “madhara makubwa” ikiwa jumuiya ya kimataifa na hasa China itashindwa kuweka shinikizo kwa utawala wa Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa kutengeneza silaha za maangamizi.

Tillerson amesema kuwa wazo la kuishambulia Korea Kaskazini kijeshi bado likol mezani, matamshi aliyoyatoa wakati akihutubia kwa mara ya kwanza kikao cha baraza la usalama la umoja wa Mataifa.

Jaribio hilo limezidisha sintofahamu kwenye peninsula ya Korea, huku utawala wa Washington na Pyongyang ukiendelea kutupiana maneno makali na vitisho kuhusu kushambuliana kijeshi.

Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye ameonya kuhusuj uwezekano wa kutokea mgogoro mkubwa kati yake na utawala wa Kim Jong-Un, amesema jaribio hilo limeenda hata kinyume na wito wa China ambaye ndie mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini kiuchumi.

Marekani imeanza kupeleka meli zake za kivita kwenye pwani ya bahari ya Korea Kusini na Kaskazini ambapo juma hili ilituma vifaa maalumu vya kudungua makombora maarufu kama THAAD, mitambo ambayo maofisa wa Marekani wamesema itaanza kufanya kazi hivi karibuni.

Korea Kaskazini hivi karibuni imefanya majaribio makubwa zaidi kuwahi kuyafanya ya makombora yake ya masafara marefu, ikisema itazamisha hata meli za Marekani baharini huku kukiwa na kila dalili kuwa huenda ikatekeleza jaribio jingine la kombora la masafa marefu.

Wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imesema kombora hilo limeshindwa baada ya kuruka umbali mfupi huku Marekani yenyewe ikisema kombora hilo limeshindwa kutoka hata nje ya ardhi ya Korea Kaskazini.