KOREA KASKAZINI-URUSI

Urusi yasema imechoshwa na majaribio ya makombora yanayotekelezwa na Korea Kaskazini

Jaribio la kombora nchini Korea Kaskazini
Jaribio la kombora nchini Korea Kaskazini KCNA via REUTERS

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema shambulizi la hivi karibuni la Korea Kaskazini kujaribu kombora lake ni hatari na linachosha.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya kusema kuwa Korea Kaskazini inaendelea kutekeleza shambulizi hili kwa sababu inachokozwa, Putin amesema  wakati umefika wa kusitisha majaribio haya.

“Hatutaki kushuhudia ongezeko la mataifa yanayomiliki na kutumia silaha za nyuklia,” amesema Putin akiwa jijini Beijing.

“Jaribio hili halifai, lina madhara mengi na ni hatari,” aliongeza Putin.

Kiongozi huyo wa Moscow amesema mbinu pekee ya kukabiliana na hali hii ni kuja katika meza ya mazungumzo na kumaliza suala hili kwa amani.

Korea Kaskazini inadai kuwa jaribio hili ni aina ya kombora jipya ambalo lina uwezo wa kubeba kiwango kikubwa cha silaha za nyuklia.

Kombora hilo lilirushwa umbali wa Kilomita 2000 kuelekea Pwani ya Japan.

Marekani na Japan zimelaani jaribio hili na kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.