INDONESIA-DINI-HAKI

Mhubiri adaiwa kueneza picha za utupu Indonesia

Waandamanaji wakifanya maombi wakati wa maandamano ya kupinga mkuu wa jiji la Jakarta  Basuki Tjahaja Purnama katika Msikiti wa  Istiqlal mjini Jakarta.
Waandamanaji wakifanya maombi wakati wa maandamano ya kupinga mkuu wa jiji la Jakarta Basuki Tjahaja Purnama katika Msikiti wa Istiqlal mjini Jakarta. © Reuters

Polisi nchini Indonesia inamtuhumu mmoja wa wahubiri wa Kiislamu wenye msimamo mkali nchini humo kuhuska katika kisa cha usambazaji wa ujumbe na picha chafu za ngono. Mhubiri huyo, ambaye kwa sasa yupo nchini Saudi Arabia, amekanusha madai hayo.

Matangazo ya kibiashara

Katika kisa cha sasa, Rizieq Shihab anadaiwa kukiuka sheria kali za kukabiliana na uenezaji wa ujumbe, picha au video chafu kwa kutuma ujumbe na picha kwa mwanaharakati Firza Husein, ambaye pia ametajwa kama mshukiwa.

Polisi wamemwita Rizieq Shihab mara kadhaa kwa mahojiano tangu Aprili lakini bado hajatii agizo la kufika kwa maafisa hao.

Bw Rizieq ambaye anafahamika sana kwa hotuba na mahubiri yake yenye ujumbe wenye kuzua utata, tayari amefungwa jela mara mbili awali kwa kuzua fujo na kuvuruga amani.

Rizieq Shihab ni kiongozi wa kundi la Islamic Defenders Front (FPI), ambalo liliongoza maandamano makubwa dhidi ya mkuuwa zamani wa mji mkuu nchi hiyo, Jakarta, Basuki Tjahaja Purnama ambaye alifungwa jela kwa kosa la kuitusi dini ya Kiislamu mwezi uliopita.

Rizieq Shihab anatuhumiwa kutuma ujumbe wenye maneno mazito ya mahaba na pia picha za utupu alipokuwa anawasiliana na mwanamke mmoja.

Wakili wa Bw Rizieq amesema madai hayo yalibuniwa na wafuasi wa Bw Purnama, anayefahamika pia kama Ahok.

Msemaji wa FPI ameambia Reuters kwamba madai hayo dhidi yake hayana msingi wowote na lengo lake ni kumhujumu mhubiri huyo.