CAMBODIA-SIASA-HAKI

Chama kikuu cha upinzani chafutwa Cambodia

Maafisa wa polisi wakitoa ulinzi mbele ya Mahakama Kuumjini Phnom Penh, Cambodia.
Maafisa wa polisi wakitoa ulinzi mbele ya Mahakama Kuumjini Phnom Penh, Cambodia. REUTERS/Samrang Pring

Mahakama ya Juu nchini Cambodia imefuta chama kikuu cha upinzani nchini humo CNRP (Cambodia National Rescue Party), na hivyo kumpa nafasi Waziri Mkuu Hun Sen kuendelea kusalia mamlakani.

Matangazo ya kibiashara

Mahakama pia imepiga marufuku wanasiasa 118 wa upinzani kufanya shughuli za kisiasa kwa kipindi cha miaka mitano.

Chama cha CNRP, ambacho kimekua na matumaini ya kumuangusha waziri mkuu, madarakani kwa zaidi ya miaka thelathini, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, kinashtumiwa kula njama ya kuipindua serikali, shutma ambazo chama hiki kinakanusha.

Wachambuzi wanaona uamuzi huu wa mahakama ni shinikizo kutoka kwa chama cha tawala dhidi ya upinzani, vyama vya kiraia na vyombo binafsi vya habari ili kunyamazisha upinzani wotewote kwa uchaguzi wa mwaka 2018 .

Kiongozi wa chama cha CNRP, Kem Sokha, alikamatwa tarehe 3 Septemba akishtumiwa kujaribu kupindua serikali ya zamani ya Khmer Rouge kwa ushirikiano na Marekani.

Binti yake, Kem Monovithya, ambaye pia ni mwanasiasa wa chama cha CNRP, amesema kuwa uamuzi huo wa mahakama haujawashangaza.

Wafadhili wa Cambodia wameomba kuachiliwa kwa Kem Sokha lakini wanaonekana kusita kuweka vikwazo dhidi ya nchi ambayo ni mshirika wa karibu wa China.

Hun Sen, katika taarifa yake iliyorushwa kwenye televisheni na kwenye Facebook, amehakikisha kwamba uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Julai mwaka ujao "utafanyika kama ilivyopangwa."

Wanasiasa wa chama cha CNRP ambao hawajapigwa marufuku kufanya shughuli yoyote ya kisiasa wana haki ya kuunda chama kipya, amesema Hun sen.