BURMA-USALAMA-HAKI

Myanmar yashtumiwa kwa ubaguzi dhidi ya jamii ya Rohingya

Wakimbizi kutoka jamii ya Rohingya katika kambi ya Bangladesh.
Wakimbizi kutoka jamii ya Rohingya katika kambi ya Bangladesh. REUTERS/Adnan Abidi

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za Binadamu la Amnesty International limetuhumu utawala wa Myanmar kwa kuendeleza ubaguzi dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na kuepelekea zaidi ya watu nusu milioni wa jamii hiyo kukimbilia Bangladesh.

Matangazo ya kibiashara

Hali ya maisha ya Warohingya waliokimbilia Bangladesh kutoka katika Jimbo la Rakhine imezua maswali mengi kwa jumuiya ya kimataifa ambayo inaeleza wazi kuwa jamii hiyo inakabiliwa na vitendo vya mauaji na ubakaji vinavyofanywa na Jeshi la Myanmar.

Mataifa hayo mawiali yamekubaliana mpango wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi waliopo Bangladesh lakini jeshi la Myanmar linapinga idadi ya wakimbizi wanaopaswa kurejea nyumbani.

Ripoti ya kurasa 100 iliyotayarishwa baada ya utafiti wa miaka miwili imetuhumu vitendo vilivyotekelezwa na Myanmar na kudai ni sawa na uhalifu dhidi ya binadamu ambao ulianza kutekelezwa miaka mitano iliyopita.

Ripoti hiyo pia inaeleza itakuwa ni vigumu kwa waislamu wa Jamii ya Rohingya kubadili mtazamo wao na kurudi Myanamar ambako wanakabiliwa na kitisho cha usalama.