KOREA KASKAZINI-MAREKANI-USALAMA

Korea Kaskazini: Tumefanikiwa kurusha kombora jipya la ICBM

Kombora la ICBM linalokwenda hadi bara jingine, ambalo limerushwa na Korea Kaskazini.
Kombora la ICBM linalokwenda hadi bara jingine, ambalo limerushwa na Korea Kaskazini. KCNA via Reuters

Korea Kaskazini imesema kuwa imefanikiwa kurusha kombora la masafa marefu la ICBM lililoruka juu zaidi na kupongeza jaribio lake hilo. Wakati huo huo Marekani kupitia Waziri wake wa Ulinzi James Mattis imesema Korea Kaskazini inaendelea kurusha makombora yanaoonekana kuhatarisha usalama duniani.

Matangazo ya kibiashara

James Mattis amesema kuwa kombora hilo liliruka juu ikilinganishwa na kombora jingine lolote lile hapo awali.

''Korea Kaskazini ilikuwa ikiunda kombora linaloweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine ambalo linaweza kurushwa eneo lolote lile duniani'', Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema.

Kwa mujibu wa maafisa wa jeshi la Korea Kaskazini, kombora hilo liliruka kwa urefu wa kilomita 4,500 na kusafiri umbali wa kilomita 960.

Korea Kaskazini imeendeleza mpango wake wa kinyuklia pamoja na ule wa utengenezaji wa makombora licha ya shutuma kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Baraza kuu la usalama la umoja wa mataifa linatarajiwa kukutana katika kikao cha dharura ili kuzungumzia hatua hiyo ya hivi karibuni.

Hata hivyo jumuiya ya kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa na Marekani wameendelea kukosoa hatua hizo za Kora Kaskazini wakitaka hatua kali zaidi zichukuliwe.

Mara ya mwisho kwa taifa hilo kulifanyia jaribio kombora lake lililokuwa la sita la nguvu za kinyuklia ni mwezi Septemba.