MAREKANI-KOREA KASKAZINI-USALAMA

Marekani yataka Korea Kaskazini kutengwa kimataifa

Nikki Haley, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Novemba 29, 2017 New York, akizungumza na mwenzake Korea Kusini, Cho Tae-yul.
Nikki Haley, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Novemba 29, 2017 New York, akizungumza na mwenzake Korea Kusini, Cho Tae-yul. REUTERS/Lucas Jackson

Serikali ya Marekani imeitaka jumuiya ya Kimataifa kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara na Korea kaskazini baada ya jaribio la hivi karibuni la Pyonyang kujaribu makombora ya masafa marefu wanayodai yanaweza kufika Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Marekani imetaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya korea kaskazini katika mkutano wa dharura ulioandaliwa na baraza la Usalama la Umoja wa mataifa ambapo pia Rais Donald Trump amemuelezea Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kama mbwa mgonjwa na kutaka vikwazo zaidi dhidi yake.

Mnamo jumatano hii Pyongyang ilifanya jaribio la kombora lenye nguvu zaidi na kukiri kuwa kombora hilo lina uwezo wa kupiga eneo lolote nchini Marekani.

Rais Kim amesema mfumo wa jaribio la silaha umeisaidia nchi yake kufikia malengo ya kuwa taifa lenye nguvu zaidi kwa silaha za nyuklia hali ambayo imesababisha hasira kwa jumuiya ya kimataifa.

Akisisitiza balozi wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Nikki Haley ametoa wito kwa mataifa yote wanachama kusitisha mahusiano yake na taifa hilo la Korea Kaskazini na kuitaja kama hatua muhimu katika kumuonya Rais Kim Jong-un, huku akieleza kuwa kama vita vitatokea basi utawala wa Kim utaangamizwa kabisa.