BOSNIA

Bosnia: Watuhumiwa 3 wa mauaji ya Waislamu wa Sebrenica wakamatwa

Ratko Mladic
Ratko Mladic REUTERS/Martin Meissner

Polisi nchini Bosnia Jumatano ya wiki hii wamewakamata watuhumiwa watatu wa mauaji ya kidini ya Sebrenica, akiwemo aliyekuwa kamanda wakati wa vita vya wenywe kwa wenyewe, wote wakidaiwa kushiriki katika mauaji ya halaiki ya Sebrenica ambapo zaidi ya waislamu 8000 waliuawa mwaka 1995, imesema ofisi ya mwendesha mashtaka.

Matangazo ya kibiashara

Mile Kosoric kamanda wa zamani wa jeshi na watuhumiwa wengine wawili wa kikosi maalumu walikamatwa magharibi mwa maeneo ya mji wa Vlasenica na Han Pijesak.

Mwendesha mashataka wa Bosnia amewaambia wanahabari kuwa watuhumiwa wote waliokamatwa sasa wanahojiwa kwa tuhuma za makosa ya kivita na kuhamasisha mauaji ya kimbari.

Mwezi Novemba mwaka huu majaji wa mahakama ya mjini The Hague Uholanzi walimuhukumu kifungo cha maisha jela aliyekuwa kamanda na mkuu wa vikosi vya Bosnia Serb, Ratko Mladic kwa kuhusika na mauaji ya Sebrenica pamoja na makosa mengine ya kivita.

Zaidi ya waislamu 8000 wanaume na vijana walichinjwa wakiwa kwenye mikono ya vikosi vilivyokuwa vinaongozwa na Mladic mashariki mwa nchi ya Bosnia mwezi Julai mwaka 1995.

Jumla ya watu laki moja waliuawa katika vita vya Bosnia kati ya mwaka 1992-1995 ambapo waislamu, Waserbia na watu kutoka Croatia walichonganishwa kupigana wakati Yugoslavia ilipokuwa ikisambaratika.

Uchunguzi wa sasa umejikita katika mauaji ya waislamu 30 ambao walitenganishwa kwenye msafara wa wakimbizi waliokuwa wakiondoka Sebrenica baada ya kuchukuliwa na vikosi vya Serb.

Mpaka sasa jumla ya miili ya waathirika elfu 6 na 733 imeshatambulika na kuzikwa, na hii ni kwa mujibu wa taasisi ya Bosnia inayotafuta wahanga wa mauaji hayo.