IRAN-USALAMA

Jeshi la Iran latangaza mwisho wa juhudi za kuhujumu serikali

Wafuasi wa serikali ya Iran wakiandamana katika mji Qom, Iran, Januari 3, 2018.
Wafuasi wa serikali ya Iran wakiandamana katika mji Qom, Iran, Januari 3, 2018. Mohammad ALI MARIZAD / AFP

Jeshi la Iran limetangaza kwamba limezima maandamano yenye vurugu ambayo yamesababisha vifo vya watu 21 na mamia kukamatwa, kando na maandamano makubwa yanayounga mkono serikali siku ya Jumatano Januari 3.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo, Iran imelalamika kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu mwenendo wa Marekani wa kuingilia masuala yake ya ndani. Iran imepuuzia mbali maandamano hayo ikiyataja kuwa yalichochewa na upinzani ukiungwa mkono na baadhi ya nchi, hasa Marekani kwa lengo la kuangusha utawala wa rais Hassan Rouhani.

"Leo tunaweza kutangaza tumefaulu kuzima uasi," alisema Mkuu wa jeshi la Mapinduzi, Mohammad Ali Jafari, akibaini kwamba idadi ya waandamanaji dhido ya serikali "walikua hawazidi 15,000 nchi kote. "

"Waliotaka kuhujumu serikali wameshindwa, " ameongeza Meja Jenerali Ali JAfari.

Alitoa tangazo hilo huku maelfu ya waungaji mkono wa serikali wakiandamana kupinga waandamanaji waliokuwa wanaipinga serikali.

Watu zaidi ya 450 wamekamatwa na maafisa wa usalama katika mji mkuu wa Tehran siku tatu zilizopita.

Maandamano ya sasa ndiyo ya kwanza makubwa zaidi tangu yaliyotokea wakati wa uchaguzi uliokuwa na utata 2009.