UNSC-KOREA KASKAZINI-USALAM-MICHEZO

Umoja wa Mataifa kujadili vikwazo dhidi ya maofisa wa Korea Kaskazini

Kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un akiambatana na maafisa wa juu ambao ni washirika wake wa karibu, Pyongyang Desemba 6, 2017.
Kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un akiambatana na maafisa wa juu ambao ni washirika wake wa karibu, Pyongyang Desemba 6, 2017. KCNA/via REUTERS

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa hii leo litaamua ikiwa liwaruhusu maofisa wa Korea Kaskazini walioko kwenye orodha ya watu waliowekewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa kusafiri kwenye Pyeongchang kushuhudia michezo ya Olimpiki akiwemo dada wa Kim Jong-Un.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya Serikali ya Korea Kusini kuwasilisha ombi rasmi kwenye baraza la usalama ikitaka kuondolewa kwa makataa ya kusafiri iliyowekwa kwa Choe Hwi ambaye ni mwenyekiti wa taifa wa kamati ya michezo wa Korea Kaskazini.

Choe aliwekewa vikwazo mwezi Juni mwaka jana kwa kuwa sehemu ya propaganda ya chama tawala cha wafanyakazi Korea Kaskazini.

Hakukuwa na pingamizi lolote la maombi hayo ya Korea Kusini, hatua inayoashiria kuwa huenda Baraza la Usalama likaunga mkono kuondolewa kwa makataa ya kusafiri kwa viongozi hao.

Wanadiplomasia wa kimataifa wanaona kuwa baraza hilo litatoa kibali bila pingamizi kwa kuwa hata mataifa mengi yameonekana kuunga mkono hatua ambayo imepigwa kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini katika kushirikiana na kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana.

Jumla ya watu 78 na makampuni 54 kwa sasa yako chini ya vikwazo vya umoja wa Mataifa ambapo wamezuiwa kusafiri na mali zao kushikiliwa.