KOREA KASKAZINI-UNSC-USALAMA

UN yaruhusu maofisa wa Korea Kaskazini kwenda Pyeongchang

Moja ya makundi ya wasanii wanaohudhuria sherehe ya uziduzi ya mashindano ya Michezo ya Olimpiki ya Pyeongchang (Februari 9-25) Februari 5, 2018.
Moja ya makundi ya wasanii wanaohudhuria sherehe ya uziduzi ya mashindano ya Michezo ya Olimpiki ya Pyeongchang (Februari 9-25) Februari 5, 2018. REUTERS/Kim Hong-Ji

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa hatimaye limetoa kibali kwa maofisa wa Korea Kaskazini walioko kwenye orodha ya vikwazo kusafiri kwenda kwenye mji wa Pyeongchang kuhudhuria ufunguzi wa michezo ya majira ya baradi la Olimpiki nchini Korea Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Hatua ya Baraza la Usalama imekuja baada ya Jumatano ya wiki hii Serikali ya Korea Kusini kuwasilisha maombi maalumu kwenye baraza hilo ikitaka maofisa wa Korea kaskazini walioko kwenye orodha ya vikwazo kuondolewa kwa muda vikwazo vya kusafiri ili kuwawezesha kuhudhuria michezo hiyo.

Mwezi Januari mwaka huu nchi ya Korea Kaskazini iliridhia kutuma ujumbe wa wanamichezo wake kwenda kushiriki michezo ya Olimpiki baada ya kuwa na mazungumzo na jirani yake Korea Kusini hatua iliyopunguza joto la mvutano baina ya nchi hizo mbili.

Miongoni mwa watu wanaotarajiwa kutoka Korea Kaskazini ni pamoja na Choe ambaye ni mkuu wa baraza la michezo na propaganda wa chama tawala cha wafanyakazi ambaye aliwekewa vikwazo na umoja wa Mataifa mwezi Juni mwaka jana.

Nchi ya Korea Kaskazini imewekewa vikwazo vya kiuchumi na silaha na umoja wa Mataifa kutokana na kuendelea na mpango wake wa kurutubisha Urani na kujaribu makombora yake ya masafa marefu.

Hakuna nchi wanachama wa Baraza la Usalama aliyepiga kura ya hapana kuidhinisha maofisa hao kuruhusiwa kwenda Korea Kusini.