URUSI

Raia wa Urusi waandamana kupinga ajali ya moto, rais Putin aonya

Rais wa Urusi Vladmir Putin akikagua eneo la tukio la ajali ya moto mjini Siberian. 27 Machi 2018.
Rais wa Urusi Vladmir Putin akikagua eneo la tukio la ajali ya moto mjini Siberian. 27 Machi 2018. Alexei Druzhinin/Kremlin via REUTERS

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema tukio la moto lililotokea kwenye mji wa Siberian lilikuwa ni uzembe, tukio ambalo limesababisha vifo vya watu 64 wakiwemo watoto 41 baada ya kujikuta wamenaswa kwenye jengo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Siku mbili baada ya tukio hilo na ukosolewaji mkubwa kupitia kwenye mitandao ya kijamii, utawala wa Kremlin umetangaza siku moja ya maombolezo ya kitaifa siku ya Jumatano huku maswali yakiibuka kuhusu hatua zilizochukuliwa na rais Putin katika kushughulikia janga hili.

Uchunguzi umeagizwa kufanyika na watu watano wanashikiliwa mpaka sasa kuhusiana na moto huo uliounguza karibu nusu ya jengo hilo lililokuwa na maduka makubwa na kumbi za Sinema.

Moto huo ulizuka kwenye maduka yaliyoko kwenye mji wa Kemerovo magharibi mwa Siberian siku ya Jumapili mchana.

Wachunguzi wanasema raia pamoja na wanyama waliungua wakiwa hai au kwa kukosa hewa kwa sababu milango ya dharula ilikuwa imefungwa, ukitolewa mfano ule wa ukumbi wa Sinema ambako watoto ndio walikuwa wengi zaidi.

Rais Putin ametembelea eneo la tukio na kuwaambia maofisa wake amechukizwa na namna kulivyokuwa na uzembe katika kukabiliana na moto huo.

“Nini kinatokea hapa? Hakuna tukio la kijeshi. Hili sio kuwa ni tukio la kuvuja kwa gesi. Watu, watoto walikuja kupumzika,” alisema rais Putin baada ya kuweka shada la maua.