IRAQ-UCHAGUZI-ISIS

Raia wa Iraq wapiga kura baada ya ushindi dhidi ya Islamic State

Zoezi la upigaji kura nchini Iraq
Zoezi la upigaji kura nchini Iraq REUTERS/Ako Rasheed

Raia wa Iraq wanapiga kura kuwachagua wabunge, uchaguzi ambao ni wa kwanza tangu kulishinda kundi la kigaidi la Islamic State.

Matangazo ya kibiashara

Ni uchaguzi ambo unatarajiwa kusaidia kuleta usalama, utulivu na amani katika taifa hilo ambalo limeendelea kukabiliana na makundi ya kigaidi kwa miaka mingi.

Usalama umeimarishwa katika maeneo mbalimbali nchini humo kuwawezesha wapiga kura, kutekeleza haki yao ya msingi.

Tume ya Uchaguzi inasema wapiga kura Milioni 24.5 wanashiriki katika Uchaguzi huu wa kihistoria.

Idadi kubwa ya raia wa Iraq wanasema, wanapiga kura kwa sababu ya usalama na uchumi, ili kuleta uthabiti katika taifa lao.

Waziri Mkuu Haider al-Abadi anatarajiwa kurejea tena ili kuongoza kwa muhula mpya, baada ya serikali yake kufanikiwa kuwashinda Islamic State katika mji wa Mosul.

Mshindi wa Uchaguzi huu anatarajiwa, kuliunganisha taifa hilo hasa baada ya kuharibiwa kwa mji wa Mosul kutokana na vita dhidi ya ugaidi.

Jumuiya ya Kimataifa tayari imesema, itatoa Dola Bilioni 30 kuisaidia nchi hiyo.