MALAYSIA-UCHUNGUZI-AJALI

Ripoti kuhusu kutoweka kwa ndege ya MH370 yazua hasiri kwa ndugu wa waathirika

Nakala za ripoti ya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa ndege ya Malaysia Airlines (MH370) mnamo mwaka 2014 huko Putrajaya, Malaysia, Julai 30, 2018.
Nakala za ripoti ya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa ndege ya Malaysia Airlines (MH370) mnamo mwaka 2014 huko Putrajaya, Malaysia, Julai 30, 2018. © AFP

Ripoti ya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa ndege ya Malaysia Airlines (MH370) iliyotoweka mnamo mwaka 2014 ikiwa na abiria 239 imekatisha tamaa na kwa familia za wahanga.

Matangazo ya kibiashara

Familia za waathirika hao walikua na matumaini kwamba ripoti ya serikali itawapa taarifa zitazowawezesha kuomboleza miaka minne baada ya kutokea kwa tukio hilo.

Lakini wakati wa mkutano wa Wizara ya Uchukuzi ya Malaysia, wakati ambapo waraka huo uliwasilishwa kwa familia za wahanga kabla ya kuchapishwa rasmi, baadhi wamekosoa ripoti hiyo ya kiufundi mbele ya viongozi.

Timu ya wachunguzi "imeshindwa kuweka wazi sababu halisi za kutoweka kwa ndege ya Malaysia Airlines (MH370)", ripoti hiyo ya kurasa 400 imehitimisha.

"Kwa kweli inakatisha tamaa, nimechanganyikiwa kabisa, hakuna jipya katika ripoti hiyo," amesema Intan Maizura Othman, ambaye mume wake alikua miongoni mwa abiria waliosafiri na Boeing 777, ambayo ilitoweka tarehe 8 Machi 2014, muda mfupi baada ya kuondoka uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur kuelekea Beijing.

Mkutano huu uligeuka kuwa wa "makabiliano makubwa" wakati ambapo ndugu wa wahanga walielezea wasiwasi wao, Bw Othman ameongeza.

"Wengi wameuliza maswali," amesema kwa upande wake G. Subramaniam, ambaye alipoteza mtoto kwenye ndege hiyo, lakini "majibu yasiyofaa yamekasirisha" familia nyingi.

Hakuna mwelekeo wa ndege uliopatikana katika eneo la utafiti wa km 120,000 km uliotazama kusini mwa Bahari ya Hindi kutoka Australia, kulingana na uchambuzi wa satelaiti ya trajectory inayowezekana ya ndege baada ya kuacha njia yake ya kinadharia.

Tafiti muhimu zaidi za baharini katika historia, zilianzishwa baada ya kutoweka kwa ndege hiyo mnamo mwaka 2014 chini ya uongozi wa Australia, kwa ushirikiano na Malaysia na China, ambapo wengi wa abiria walikua ni kutoka nchi hizo. Hata hivyo tafiti hizo zilisitishwa mnamo mwezi Januari 2017.

Karibu vipande 20 vya ndege hiyo ya Malaysia Airlines viliokotwa katika Bahari ya Hindi, katika pwani Afrika Mashariki, mbali na eneo la uchunguzi - vilitambuliwa, na mamlaka walidai kwamba labda vipande hivyo vilikua vya ndege hiyo iliyotoweka. Lakini mpaka sasa ukweli haujajulikana kuhusu sababu za kutoweka kwa ndege hiyo.