CHINA-CAMBODIA-USHIRIKIANO

China yaonya nchi yoyote ya kigeni kuingila masuala ya Cambodia

Afisa mwandamizi wa China amempongeza Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Sen kwa ushindi wa chama chake katika uchaguzi wa wabunge wa Jumapili.

Viongozi wanachunguza orodha ya wapigakura katika kituo cha uchaguzi cha Phnom Penh huko Cambodia, Julai 28, 2018.
Viongozi wanachunguza orodha ya wapigakura katika kituo cha uchaguzi cha Phnom Penh huko Cambodia, Julai 28, 2018. REUTERS/Darren Whiteside
Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo imeonya nchi yoyote kuingilia uchaguzi huo baada ya upinzani kudai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu mkubwa, huku nchi za magharibi zikiendelea kukosoa utawala wa nchi hiyo.

China ni mshirika mkuu wa kiuchumi na kidiplomasia wa Cambodia.

Chama cha CCP kinachoongozwa na Hun Sen, aliyekuwa askari wa Khmer Rouge, kilitangaza kuwa kilishinda viti 125 katika uchaguzi wa wabunge, uchaguzi ambao chama kikuu cha upinzani cha PSNC hakikushiriki baada ya kuvunjwa mwaka uliyopita. Naibu kiongozi wa PSNC alitaja uchaguzi huo kama "kifo cha demokrasia".

Mjumbe wa serikali ya China Wang Yi, mwanadiplomasia wa juu katika nchi hiyo, amesema katika taarifa kwamba uchaguzi ulikuwa ni udhihirisho katika "kuunga mkono" na "kuwa na imani" na chama cha CCP.

"China imekuwa ikisaidia jitihada za Cambodia kulinda uhuru wake, amani na utulivu, na inapinga nchi yoyote kuingilia kati katika masuala ya ndani ya Cambodia," ameandika.

Marekani imetangaza kwamba inapanga kuchukua vikwazo vipya dhidi ya serikali ya Phnom Penh, ikiwa ni pamoja na kunyimwa vya visa kwa baadhi ya mawaziri. Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umetishia kuishukulia Cambodia vikwazo vya kiuchumi tangu chama cha PSNC kupigwa marufuku.