INDONESIA-MAJANGA YA ASILI

Tetemeko la ardhi laua watu zaidi ya 90 Indonesia

Wagonjwa katika Hospitali ya Mataram huko Lombok walihamishwa kutoka kituo cha magari cha hospitali hiyo baada ya tetemeko la ardhi Agosti 5.
Wagonjwa katika Hospitali ya Mataram huko Lombok walihamishwa kutoka kituo cha magari cha hospitali hiyo baada ya tetemeko la ardhi Agosti 5. Antara Foto/Ahmad Subaidi/ via REUTERS

Serikali ya Indonesia imetangaza kwamba zaidi ya watu 82 wamefariki dunia baada kisiwa cha Lombok kukumbwa na tetemeko kubwa la ardhi. Tetemeko hilo lenye nguvu ya 7 katika vipimo vya Richter limeharibu vibaya miundombinu ya umeme na barabara. Pia nyumba nyingi zimeathirika.

Matangazo ya kibiashara

Tetemeko hili limekuja wiki moja baada ya jingingine kuipiga sehemu hiyo ya Lombok, kisiwa maarufu kwa shughuli za utalii ambapo watu 16 waliuawa.

Maafisa wa idara ya kudhibiti majanga wanasema mamia ya watu wamejeruhiwa vibaya kwa tukio hilo lililotokea Jumapili.

Msemaji wa idara ya kudhibiti majanga ya Indonesia amesema nyumba nyingi zimeathirika vibaya, ambapo nyingi kati ya hizo zilijengwa kwa kutumia nyenzo duni.

Rais wa Indonesia Joko Widodo amesema serikali yake inafanya jitihada za kutosha kunusuru maisha ya majeruhi huku akituma salam za rambirambi kwa familia za wafiwa.

Katika kisiwa jirani cha Bali picha za video zimeonyesha watu wakikimbia majumbani mwao huku wakiomba msaada.

Indonesia imeendelea kukumbwa na majanga mbalimbali na kusababisha watu wengi kupoteza maisha na wengine kulazimika kuyahama makaazi yao.