Seoul na Pyongyang kuzungumza kabla ya mkutano wa marais
Imechapishwa:
Wawakilishi kutoka Seoul na Pyongyang wanakutana Jumatatu wiki hii kwa mazungumzo ya ngazi ya juu, kabla ya mkutano kati ya viongozi wa pande zote mbili za rasi ya Korea, gazeti la kila siku la Korea Kusini la Kookmin Ilbo limeripoti.
Kim Jong-un, kiongozi wa Korea Kaskazini, na Moon Jae-in, rais wa Korea Kusini, walikutana mwezi Aprili na walikubaliana kuandaa mkutano katika majira ya baridi huko Pyongyang.
Gazeti la kila siku la Kookmin Ilbo likinukuu afisa mwandamizi wa Korea Kusini, limeripoti kwamba mkutano huo unatarajiwa kufanyika kabla ya mwishoni mwa mwezi Agosti.
Msemaji wa Moon Jae-in alisema siku ya Jumapili kuwa ofisi ya rais wa Korea Kusini ina imani kuwa tarehe ya mkutano huo inaweza kujadiliwa Jumatatu wiki hii.
"Tunatarajia kuwa tarehe, eneo na wajumbe katika mkutano huo wa kihistoria vinaweza kujadiliwa leo Jumatatu," msemaji wa rais amesema bila kutoa maelezo zaidi.