BURMA-UN-USALAMA

UN yashtumu uongozi wa jeshi Burma kuhamasisha mauaji ya kimbari

Jeshi la Burma lilitekeleza mauaji na ubakaji dhidi watu kutoka jamii ndogo ya Rohingya na "kupanga mauaji ya halaiki" kwa mujibu wa tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa katika ripoti yake ya mwisho iliyotolewa leo Jumatatu. 

Vijiji walipokua wakiishi watu kutoka jamii ya Rohingya, vilivyochomwa moto, Burma.
Vijiji walipokua wakiishi watu kutoka jamii ya Rohingya, vilivyochomwa moto, Burma. REUTERS/Michelle Nichols
Matangazo ya kibiashara

Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa inaomba kiongozi mkuu wa "Tatmadaw" (jeshi) na majenerali wengine watano kufunguliwa mashitaka haraka iwezekanavyo.

Serikali ya kiraia inayoongozwa na Aung San Suu Kyi imeruhusu hotuba ya chuki kuendelea kusambaa, imeharibu nyaraka, na haikuonyesha wajibu wake wa kulinda jamii ya watu wachache dhidi ya uhalifu kama vile uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa na askari huko Rakhine, Kachin na Shan, wamehitimisha wachunguzi huru wa Umoja wa Mataifa katika ripoti yao. "Kwa hiyo serikali ya Burma imechangia kutekelezwa kwa maovu haya".

Jeshi la Burma lilizindua operesheni iliyosababisha vifo vingi mwaka mmoja uliopita katika Jimbo la Rakhine (Arakan) katika kukabiliana na mashambulizi ya kundi la waasi la ARSA, dhidi ya vituo zaidi ya thelathini vya polisi na jeshi.

Watu 700,000 kutoka jamii ya Rohingya wamekimbia ukandamizaji ulio kua ukitekelezwa na jeshi.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inabaini kuwa hatua za kijeshi, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa vijiji, haziendani kabisa na hali halisi ya vitisho."

"Uhalifu katika Jimbo la Rakhine, na jinsi uliofanyika, unafanana, madhara yake na malengo yake kwa wale ambao waliruhusu mpango wa mauaji ya halaiki kutekelezwa katika maeneo mengine ya nchi" imebaini timu ya wataalamu huru ya Umoja wa Mataifa, inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Indonesia Marzuki Darusman.

"Kuna taarifa za kutosha kuanzisha kesi dhidi ya viongozi waandamizi katika uongozi wa Tatmadaw (jeshi) ili mahakama husika kuamua kuhusika kwao katika mauaji ya kimbari", wanasema wachunguzi katika ripoti hii ya mwisho yenye kurasa 20.

Serikali ya Aung San Suu Kyi imefutilia mbali baadhi ya shutma dhidi ya vikosi vya usalama. Serikali imejenga vituo vya kuwapokea wapkimbizi wa Rohingya wanaotaka kurudi katika Jimbo la Rakhine. Lakini mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasema wakimbizi hawawezi kurudi kwa sababu ya usalama.

Wachunguzi wanaomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa wahusika wote wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Wameomba kufungua mashitaka mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC au kuunda mahakama maalum.