UN-CHINA-SAUDI ARABIA-MAREKANI-EU

Bachelet azionya China, EU, Marekani na Saudi Arabia

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet. (Picha ya kumbukumbu).
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet. (Picha ya kumbukumbu). REUTERS/Lucas Jackson

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu Michelle Bachelet ameitolea wito China kuruhusu waangalizi kuingia nchini humo kufuatia "taarifa za kutisha" kuhusu watu kutoka jamii ya Wawghur wanaozuiliwa katika kambi zisizojulikana katika mkoa wa Xinjiang.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa zamani wa Chile, ambaye ametoa hotuba yake ya kwanza mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, ametangaza pia kwamba kuna timu ambazo zinatarajiwa kutumwa nchini Austria na Italia kuhusu kwalinda wahamiaji.

Amesema pia kuwa ana wasiwasi kwamba watoto 500 wahamiaji waliotenganishwa na wazazi wao walipowasili nchini Marekani bado hawajapatikana.

Bachelet pia ameutaka muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen kuwa na uwazi zaidi katika operesheni zake na ameiomba nchi hiyo kutoa maelezo kuhusu wahusika wa mashambulizi ya anga yaliyosababisha vifo dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na shambulizi dhidi ya basi ndogo iliyokuwa ikibeba watoto huko Saada mwezi uliopita.

Pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatima ya watu kutoka jamii ndogo ya Waislamu ya Rohingya nchini Burma ambapo watu 700,000 kutoka jamii hiyo walikimbilia Bangladesh kufuatia operesheni ya kijeshi ya ukandamizaji mkubwa baada ya machafuko ya wanaharakati wanaotaka kujitenga kwa eneo lao.

Pia ameshukuru jitihada za nchi wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kuweka mfumo huru wa kimataifa kwa mapokezi, mshikamano, kuhifadhi na kuchambua ushahidi wa uhalifu mkubwa zaidi wa kimataifa ili kuwezesha kesi kushughulikiwa bila kuegmea katika mahakama za nchi mbalimbali na za kimataifa.

"Utaratibu huu, sawa na ule ulioanzishwa kuchunguza uhalifu wa vita nchini Syria, utaongeza na kuwezesha kazi ya waendesha mashitaka wa ICC", Michelle Bachelet ameongeza.