CHINA-USALAMA

Dereva wa gari ndogo agonga umati wa watu China, kumi na moja wafariki dunia

Polisi wa China wakitoa ulinzi.
Polisi wa China wakitoa ulinzi. REUTERS/Tyrone Siu

Watu kumi na mmoja wamepoteza maisha na wengine 44 wamejeruhiwa na mtu mmoja aliyeingiza gari lake kwa kasi katika umati wa watu katika eneo linalotembelewa na watu wengi kusini mwa China.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya tukio, dereva huyo aliwashambulia wapita njia kwa kisu na koleo, chanzo cha polisi kimesema.

Serikali imelichukulia tukio hilo kama kitendo cha mtu aliyepungukiwa na akili ambaye alitaka "kulipiza kisasi kwa jamii" baada ya kuhukumiwa mara nyingi kwa kosa la biashara ya madawa ya kulevya, wizi na unyanyasaji.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi wiki hii huko Mishui, mkoani Hunan, serikali katika mkoa huo imesema katika taarifa yake.

Dereva, aliyefahamika kwa jima moja tu la Yang, amekamatwa na kufungwa, serikali imeongeza.

Tukio hili linakumbusha shambulio lililoendeshwa katika eneo la Tiananmen huko Beijing mnamo mwaka 2013, shambulio ambalo mamlaka ilihusisha wanaharakati wa Kiislamu kutoka Xinjiang wanaotaka kujitenga kwa eneo lao.