Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran vyaanza kutumika
Imechapishwa:
Serikali ya Iran imesema haitishwi na hatua ya Marekani ya kuiwekea nchi hiyo vikwazo zaidi, kauli inayotolewa wakati huu ambapo utawala wa Washington leo Jumatatu umetangaza vikwazo vipya kwa nchi hiyo.
Siku ya Jumapili maelfu ya raia wa Iran waliandamana jijini Tehran kukashifu kile ambacho walisema ni vitisho vya Marekani dhidi ya uhuru wa taifa hilo, huku kiongozi wa kidini wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamenei akisisitiza nchi yake haitatetereka.
Serikali ya Marekani imetangaza kuwa leo Jumatatu itarejesha vikwazo vitakavyolenga sekta ya mafuta na ile ya kifedha, vikwazo ambavyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema ni vikwazo vigumu zaidi kuwahi kuvichukua.
Vikwazo hivi vinarejeshwa ikiwa ni miezi michache imepita tangu rais Donald Trump afanye uamuzi tata wa kuiondoa nchi yake kwenye mkataba wa nyuklia uliotiwa saini kati ya Iran na mataifa yenye nguvu.
Licha ya kutengwa na Marekani nchi ya Iran inaungwa mkono na mataifa mengi ambayo yamesalia kwenye mkataba huo.