JAPAN-NISSAN-MITSUBISHI-UCHUMI

Carlos Ghosn kuendelea kuzuiliwa siku 10

Mahakama ya Japan imetoa uamuzi wa kuendelea kumzuia siku kumi jela mwenyekiti wa muungano wa makampuni Renault-Nissan-Mitsubishi Motors, Carlos Ghosn, anayeshtumiwa matumizi mabaya ya fedha.

Jela kuu la Tokyo, ambapo Carlos Ghosn anafungwa, Novemba 30, 2018.
Jela kuu la Tokyo, ambapo Carlos Ghosn anafungwa, Novemba 30, 2018. REUTERS/Issei Kato
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo ulitolewa Ijumaa hii, Novemba 30 na Mahakama ya Wilaya ya Tokyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Japan. Hatua kama hiyo pia imechukuliwa dhidi ya Greg Kelly, meneja wa zamani wa Nissan na mshirika wa karibu wa tajari huyo Mfaransa. Carlos Ghosn alikamatwa Novemba 19 huko Tokyo kwa kesi ya kuficha mapato na matumizi mabaya ya mali ya kampuni.

Carlos Ghosn atasaliai kizuizini katika jela ya Tokyo mpaka Desemba 10. Kwa tarehe hiyo, anaweza kuachiliwa huru iwapo hatapatikana na hatia au kushtakiwa, na kwa hilo huenda akaachiliwa huru kwa dhamana au kufungwa.

Carlos Ghosn anashtumiwa kutoa taarifa ya kiwango cha chini cha mapato yake katika kampuni ya Nissan, sawa na euro milioni 7.7 kwa mwaka kwa jumla ya miaka mitano au miaka mitatu hadi minne, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Japan. Kwa hiyo majaji wa Japan wanaweza kupanua uchunguzi wao kwa miaka mingine au sababu nyingine na kumkamata tena Carlos Ghosn. Kwa hiyo mchakato wa kuzuiliwa jela utaendela kujirudia.

Hata hivyo tajarihuyo Mfarasa amekanusha madai hayo yanayomkabili. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Japan na shirika la Habari la Reuters, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wanaweza kujadili suala la Carlos Ghosn kando ya Mkutano wa G20 nchini Argentina.