MAREKANI- KOREA KASKAZINI-VIETNAM-USHIRIKIANO

Vietnam yajiandaa kuwapokea Kim Jong-un na Donald Trump

Maafisa wa polisi wa Vietinam jini Hanoi, Februari 24, 2019 mbele ya bendera za Korea Kaskazini na Marekani.
Maafisa wa polisi wa Vietinam jini Hanoi, Februari 24, 2019 mbele ya bendera za Korea Kaskazini na Marekani. Jewel SAMAD / AFP

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, yuko njiani kwenda Vietnam, ambako anatarajiwa kukutana na rais wa Maekani Donald Trump. Wawili hao hawajakutana tangu mkutano wao wa kwanza mnamo mwezi Juni 2018 huko Singapore.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Marekani ameendelea kukaribisha uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili na maendeleo yaliyofikiwa katika mpango wa kuondokana na silaha za nyuklia nchini Korea Kaskazini.

Bendera za Marekani na Korea Kaskazini zimewekwa katika maeneo mbali mbali ya mji mkuu wa Vietnam, Hanoi.

Msafara wa magari ya kijeshi wa Kim Jong-un umevuka mpaka wa China na utachukua siku mbili kuwasili Vietnam. Haijulikani ni lini wawili hao watakutana. Lakini Donald Trump na Kim Jong-un wanatarajia kukutana Jumatano wiki hii, kwa mujibu wa mwandishi wetu Hanoi, Stephane Lagarde.

Ishara za uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili zinaonekana. Tangu mkutano wa Singapore, Korea Kaskazini imesitisha majaribio yake ya makombora ya masafa marefu, Mateka wa Marekani walirejeshwa nyumbani na miili ya askari wa Marekani waliouawa wakati wa Vita Kuu ya Korea ilirejeshwa nchini Marekani.

Ishara, ambayo Rais wa Marekani anaona kuwa ni nafasi nzuri ya kufikia mkataba wa kuachana na mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.