IRAN-SIASA

Waziri wa mambo ya nje wa Iran ajiuzulu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif katika mkutano na waandishi wa habari, Tehran Februari 13, 2019.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif katika mkutano na waandishi wa habari, Tehran Februari 13, 2019. ATTA KENARE / AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ambaye kwa sehemu kubwa alifanikisha mazungumzo ya nchi yake kufikia muafaka na nchi za magharibi kuhusu mpango wake wa nyuklia, ametangaza kujiuzulu nafasi yake.

Matangazo ya kibiashara

Kujizulu kwa waziri Zarif kumewashtua wanadiplomasia wengi ambao walimuona kama mtu mwenye ushawishi kwa mataifa ya magharibi, uamuzi ambao hata hivyo unasubiri baraka za rais Hassan Rouhani.

Kupitia kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Instagram, waziri ZARIF amewashukuru wananchi wa taifa hilo na nchi washirika kwa kumuamini huku akiomba radhi kwa kushindwa kuendelea na kazi aliyoaminiwa na taifa.

Uamuzi wake wa kujizulu umekuja saa chache tu baada ya ziara ya kushtukiza ya rais wa Syria Bashar Al-Assad mjini Tehran, ambapo inaripotiwa kuwa hakuwepo hata katika mkutano kati yake na kiongozi wa juu wa kidini wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamanei pamoja na rais Rouhani.

Mpaka sasa haijafahamika wazi sababu zilizomsukuma waziri Zarif kujiuzulu nafasi yake.