AMNESTY INTERNATIONAL-HAKI ZA BINADAMU

Ripoti: Utekelezaji wa adhabu ya kifo ulipungua kwa kiasi kikubwa mnamo mwaka 2018

Amnesty inalaani kuongezeka kwa mauaji kufuatia adhabu ya kifo nchini Iran.
Amnesty inalaani kuongezeka kwa mauaji kufuatia adhabu ya kifo nchini Iran. REUTERS/Morteza Nikoubazl

Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International limebaini kwamba adhabu ya kifo ilipungua kwa asilimia kubwa mnamo mwaka 2018.

Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti yake shirika hilo limesema kuwa mnamo mwaka 2018 liliorodhesha angalau watu 690 walionyongwa katika nchi 20, ikiwa ni sawa na chini ya asilimia 31 ikilinganishwa na mwaka 2017, kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa, kulingana na ripoti ya kila mwaka kuhusu adhabu ya kifo iliyotolewa leo Jumatano Aprili 10, 2019.

Watu wengi walinyongwa nchini China, Iran, Saudi Arabia, Vietnam na Iraq.

Idadi hiyo inaweza kuwa kubwa nchini China, limebaini shirika hilo.

Mbali na China, nchi nne zinachukua asilimia 78 ya watu walionyongwa duniani kote: Iran, Saudi Arabia, Vietnam na Iraq.

Iraq, Pakistan na Somalia pia zinaonyesha kuwa utekelezaji wa adhabu ya kifo umepungua kwa kiasi kikubwa kwa mwaka 2018.

Hata hivyo baadhi ya nchi, kama vile Belarus, Marekani, Japan, Singapore na Sudan Kusini wametekeleza adhabu ya kifo na kuua watu wengi, imesema Amnesty International.

Thailand imetekeleza adhabu hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009. Rais wa Sri Lanka Maithripala Sirisena, hivi karibuni alisema anataka kurejelea adhabu ya kifo baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita, Amnesty International imeongeza.

Mfalme wa Brunei aliahidi mwanzoni mwa mwezi Aprili kuwa watu watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, uzinzi watakabiliwa na adhabu ya kifo.