MAREKANI-IRAN-USALAMA

Donald Trump: Hatutokubali Iran kuendelea kuwa tishio la ulimwengu

Rais wa Marekani Donald Trump wakati akitoa hotuba katika mji wa Panama, Florida, Mei 8, 2019.
Rais wa Marekani Donald Trump wakati akitoa hotuba katika mji wa Panama, Florida, Mei 8, 2019. REUTERS/Kevin Lamarque

Mwaka mmoja baada ya Marekani kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran, serikali ya Washington imeweka vikwazo vipya dhidi ya serikali ya Tehran.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hizi zinakuja wakati Iran imetangaza kwa upande wake kwamba itasitisha kutekeleza "baadhi" ya "ahadi zake" ilizotoa katika mfumo wa makubaliano ya kimataifa juu ya mpango wake wa nyuklia wa mwaka 2015, kufutia hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye mkataba huo.

Vikwazo hivi vipya vya Marekani vinahusu chuma, aluminium na shaba kutoka Irani. Kwa mujibu wa Donald Trump, hivi ni vyanzo vikuu vya mapato ya nje vya Irani, baada ya mafuta ambayo tayari yanakabiliwa na vikwazo vya Marekani. "Sera ya Marekani bado inazuia Iran kuendeleza silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu, na kukabiliana na ushawishi mkubwa wa Iran Mashariki ya Kati," sheria ya rais Trump aliyotia saini Jumatano inasema.

Nchi ya Iran kwa upande wake imetangaza kuwa itaanza kurutubisha tena Uranium kwa kiwango cha juu ikiwa nchi za magharibi zitashindwa kuheshimu makubaliano ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.

Katika hotuba yake kwa taifa rais wa Iran, Hassan Rouhani amesema anatoa siku 60 kwa mataifa 5 yaliyosalia kwenye mkataba wa mwaka 2015 kutimiza ahadi zao za kulinda mafuta yake na sekta za kifedha dhidi ya vikwazo vya Marekani.