MAREKANI-IRAN-UFARANSA-USHIRIKIANO-USALAMA

Mpango wa nyuklia wa Iran: Ufaransa yataka kuwa mpatanishi kati ya Tehran na Washington

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mei 17, 2019.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Mei 17, 2019. Iroz Gaizka/Pool via REUTERS

Ufaransa imeendelea kujikita katika masuala ya nyuklia ya Iran, baada ya kuibuka vita vya maneno kati ya Iran na Marekani kufuatia hatua ya Iran kuendelea kurutubisha madini ya uraniamu kwa kiwango cha juu zaidi.

Matangazo ya kibiashara

Mshauri wa Emmanuel Macron anayehusika na masuala ya kidiplomasia, Emmanuel Bonne, anazuru Iran leo Jumanne wakati nchi hiyo inayoendelea kubanwa na vikwazo vya Marekani imetangaza tu kwamba imezidisha kiwango cha uboreshaji wa uranium kiliyowekwa na makubaliano kuhusu nyuklia yaliyotiliwa saini mwaka 2015.

Kazi ni ngumu, lakini Ufaransa haina njia nyingine, kati ya Iran na Marekani, itailazimu tu kutuliza mvutano huo unaoendelea. "Ufaransa imejikubalisha kuingilia kati na kuzima mara moja mvutano huo unaoendelea," chanzo cha kidiplomasia kimebaini. Kituo cha mawasiliano kinaendelea na kazi yake na Rais Emmanuel Macron anafanya mazungumzo yenye ubora kwa upande wa Marekani na upande wa Iran, chanzo hiki kimeongeza.

Umoja wa Ulaya umeelezea wasi wasi wake juu ya mipango ya Iran ya kuanza tena kurutubisha madini ya Uranium ya kuiwezsha nchi hiyo kuunda silaha za nyuklia. Iran ilianza kuyarutubisha madini hayo Jumatatu wiiki hii hadi kufikia asilimia 4.5 na kukiuka mkataba uliyofikiwa mnamo mwaka 2015 na mataifa makubwa.

Umoja wa Ulaya umesema mkataba uliofikiwa na Iran ndiyo njia pekee ya ufanisi ya kuzuia uundaji wa silaha za nyuklia

Umoja wa Ulaya umeitaka Iran iache kuchukua hatua zozote za kukiuka mkataba. Msemaji wa Umoja wa Ulaya Maja Kocijancic ameeleza kwamba Umoja huo unasubiri ripoti ya shirika la kudhibiti nishati ya nyuklia kabla ya kuchukua hatua.