IRAN-MAREKANI-VIKWAZO-USALAMA

Iran: Paris, Berlin na London watoa wito wa kukomesha mvutano katika Ghuba

Katika taarifa ya pamoja, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wameelezea wasiwasi wao kufuatia kuongezeka kwa mvutano na vita vya maneno vinavyoendelea kati ya Iran na Marekani.

Theresa May, Emmanuel Macron na Angela Merkel, Juni 8, 2018 La Malbaie, Canada.
Theresa May, Emmanuel Macron na Angela Merkel, Juni 8, 2018 La Malbaie, Canada. GEOFF ROBINS / AFP
Matangazo ya kibiashara

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wamesema wana wasiwasi kwamba makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran "yatazorota" kwa sababu ya vikwazo vilivyowekwa na Washington na hatua ya Tehran ya kutotekeleza baadhi ya ibara za makubaliano hayo.

Katika taarifa yao ya pamoja, nchi hizo tatu, ambazo zilitia saini kwenye makubaliano ya Vienna, zimebaini kwamba Iran imekuwa inaheshimu ahadi zake wakati Marekani ilitangaza kwamba inajiondoa kwenye mkataba huo na kuamua kurejesha vikwazo. Ikiwa mvutano umeshindwa kudhibiiwa kati ya nchi hizo mbili na kuwa usalama katika bahari ya Ghuba la Kiajemi umeendelea kudorora, ni kwa sababu ya uamuzi wa Marekani, nchi hizo tatu za Ulaya zimebaini.

Hata hivyo, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wametoa wito kwa Iran kubadilisha maamuzi yake ya hivi karibuni ya kuhifadhi na kuimarisha uranium kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko kile ambacho iliruhusiwa.

Mwaka mmoja baada ya Marekani kujiondoa kwenye mkataba wa kimataifa kuhusu ukomo kwenye mpango wa nyuklia wa Iran, Iran iliamua mnamo mwezi Mei kuacha kupunguza akiba yake ya maji mazito na uranium yenye utajiri.

Siku ya Jumatatu, Julai 8, Tehran ilitangaza kwamba sasa itazalisha uranium yenye utajiri kwa kiwango cha angalau 4.5%, kiwango kilichokatazwa.

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wametoa wito wa kukomeshwa kwa mvutano unaondelea na kuendelea na mazungumzo. "Nchi zetu hivi karibuni zimechukua mipango kadhaa ya kidiplomasia ili kuchangia kupkomesha mvutano na kuendeleza mazungumzo, ikiwa ni nji tosha zinazohitajika kwa haraka," taarifa hiyo imebaini.