INDONESIA-MAJANGA ASILI

Tetemeko la ardhi laua mtu mmoja na kuharibu mamia ya nyumba Indonesia

Mtu mmoja amefariki dunia na mamia ya nyumba kuharibiwa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga mashariki mwa Indonesia, kwa mujibu wa ripoti awali iliyotolewa Jumatatu jioni.

Tetemeko la ardhi lasababisha maafa Indonesia.
Tetemeko la ardhi lasababisha maafa Indonesia. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Tetemeko hilo la ardhi lilitokea muda mfupi baada ya saa 12:00 jioni kaskazini mwa rasi ya Maluku, kwenye kina cha kilomita 10, na kusababisha hofu kwa wakazi na kulazimika kutoroka makaazi yao.

Kitovu cha tetemeko hilo kiligundulwa kilomita 165 kusini mwa Ternate, jiji kuu la kaskazini mwa Maluku.

"Mtu huyo aliyefariki dunia aliangukiwa na vifusi wakati nyumba yake ilipoporomoka," Ihksan Subur, afisa wa idara ianayokabiliana na majanga katika eneo hilo ameliambia shirika la Habari la AFP. Hakuna majeruhi mengine yaliyoripotiwa licha ya ukubwa wa tetemeko hili la ardhi.

Mamia ya watu walikimbilia katika maeneo salama kama vile shule na majengo ya serikali.

"Raia wanaendelea kuwa na hofu ya kutokea tetemeko jingine, na ndio sababu wamegoma kurejea makwao," amesema afisa huyo.