CHINA-MAREKANI-BIASHARA-UCHUMI

China na Marekani wakubaliana kutafutia suluhu matatizo kati yao

Naibu Waziri Mkuu wa China Liu He, amezungumza kwa simu na mwakilishi wa biashara wa Marekani Robert Lighthizer na Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin kuhusu Masuala ya "awamu ya kwanza" katika mkataba wa biashara, Wizara ya Biashara ya China imbaini.

China na Marekani, nchi mbili zilizostawi kiuchumi duniani, zinaendelea na mazungumzo baada ya kuibuka mvutano wa kibiashara.
China na Marekani, nchi mbili zilizostawi kiuchumi duniani, zinaendelea na mazungumzo baada ya kuibuka mvutano wa kibiashara. REUTERS/Jason Lee
Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake, Wizara ya Biashara ya China imesema pande zote mbili pia zimejadili masuala nyeti na kufikia makubaliano ya kutatua matatizo kati ya nchi hizo.

Liu He, kiongozi mkuu wa ujumbe wa Beijing katika masuala ya biashara, na wenzake kutoka Marekani wamekubaliana kuendelea na mazungumzo kuhusu masuala nyeti yaliyosalia mezani.

Mapema Jumanne hii Gazeti la Global Times, likinukuu wataalamu walio karibu na serikali ya China, limeripoti kwamba China na Marekani kwa pamoja walikuwa wamekubaliana kuhusu awamu ya kwanza ya mkataba wa biashara.

Siku ya Ijuma ya wiki iliyopita Rais wa Marekani, Donald Trump alisema kuwa nchi hizi mbili zilizostawi kiuchumi duniani ziko "karibu" kutia saini kwenye mkataba ili kumaliza mzozo wao wa kibiashara.

Mwenzake wa Uchina Xi Jinping alisisitiza utayari wa China kukamilisha makubaliano ya kibiashara na Marekani lakini alisema hatosita kuchukua hatua ikiwa itahitajika.

Wiki iliyopita Wataalamu wanaofuatilia kwa karibu faili hii na watu walio karibu na ikulu ya White House walisema kwamba zoezi la kutia saini kwenye mkataba wa biashara kati ya China na Marekani linaweza kufanyika mwaka ujao kutokana na mvutano unaoendelea katika mazungumzo ya sasa.