MAREKANI-KOREA KASKAZINI-USHIRIKIANO

Beijing, Seoul na Tokyo kuendeleza mazungumzo kati ya Marekani na Korea Kaskazini

Rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wakisaini hati ya pamoja katika Hoteli ya Capella kwenye kisiwa cha Sentosa, Singapore, Juni 12, 2018.
Rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wakisaini hati ya pamoja katika Hoteli ya Capella kwenye kisiwa cha Sentosa, Singapore, Juni 12, 2018. REUTERS / Jonathan Ernst

China, Korea Kusini na Japan zimekubali kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendeleza mazungumzo kati ya Washington na Pyongyang, Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesema Jumanne wiki hii baada ya mkutano wa kilele wa nchi hizo tatu huko Chengdu , kusini magharibi mwa China.

Matangazo ya kibiashara

Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wamekutana mara tatu tangu Juni 2018, lakini hatua kidogo imepigwa katika mazungumzo kuhusu kuvunjwa kwa mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

'Korea Kusini, China na Japan zimekubaliana kuendelea na mawasiliano ya karibu na ushirikiano kutoka pande zote tatu kwa lengo la kurejesha usalama na kuleta amani ya kudumu kwenye rasi ya Korea," amesema Moon Jae-in wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mawaziri wakuu wa China na Japan - Li Keqiang na Shinzo Abe.

'Tunakubaliana kuhusu hoja ya kwamba amani katika rasi ya Korea ni kwa faida ya nchi hizi tatu na tumeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa usalama na amani vinaendelea kupitia mazungumzo ya haraka kati ya Korea Kaskazini na Marekani, 'ameongeza.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa China Li Keqiang, amesema viongozi hao watatu wamethibitisha tena haja ya kupata suluhisho kwa suala la Korea Kaskazini kupitia mazungumzo.

China ni msaidizi mkuu wa Korea Kaskazini kwenye ngazi ya kimataifa.

Mjumbe Maalum wa Marekani nchini Korea Kaskazini Stephen Biegun alikutana kwa mazungumzo na wanadiplomasia wawili wa China wakati wa ziara yake ya siku mbili huko Beijing wiki iliyopita baada ya mfululizo wa mikutano kama hiyo nchini Korea Kusini na Japan siku chache zilizopita.

Wiki iliyopita China na Urusi ziliwasilisha azimio la rasimu kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo inapendekeza kuondoa vikwazo kadhaa vilivyowekwa dhidi ya Korea Kaskazini 'kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya raia '.