IRAN-MAREKANI-USALAMA

Paris, Berlin na London zaitaka Iran kuheshimu mpango wa nyuklia

Kutoka kushoto kwenda kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Kutoka kushoto kwenda kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. REUTERS

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson wameitaka Iran kuachana na vitendo vyovyote hatari.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi hao watatu wameiomba Iran kuheshimu kikamilifu ahadi zake katika Mpango wa hatua kamili za pamoja(JCPoA), kulingana na taarifa kutoka kwa viongozi hao watatu iliotumwa na Elysée.

Tehran iliahidi kulipiza kisasi kifo cha Jenerali Qassem Soleimani, aliyeuawa siku ya Alhamisi usiku katika shambulizi la anga la Marekani mjini Baghdad nchini Iraq.

Siku ya Jumapili Iran ilitangaza kwamba itajiondoa kwenye mpango wa nyuklia uliofikiwa mwaka 2015 na kwamba itakiuka kiwango cha urutibishaji wa madini ya Uranium kilichowekwa katika makubaliano ya nyuklia ya mnamo 2015 yalioidhinishwa na mataifa yenye nguvu duniani.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeionya Iran dhidi ya hatua hiyo inayokwenda kinyume na makubaliano hayo.

" Ni muhimu kusitisha uhasama. Tunatoa wito kwa pande zote kuchukua hatua za kujizuia na kuwa na majukumu. Hali ya sasa wa vurugu nchini Iraq inapaswa kusitishwa," imesema taarifa hiyo.

"Tunatoa wito kwa Iran kujiepusha na vitendo vyovyote hatari au na tunaiomba kuheshimu kikamilifu ahadi zake katika Mpango wa hatua kamili za pamoja."