MAREKANI-IRAN-USALAMA-HAKI

Afisa mstaafu wa FBI afariki dunia katika jela Iran

Robert Levinson, afisa wa shirika la ujasusi la Marekani (FBI), ambaye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha mwaka 2007 nchini Irani, "amefariki dunia akiwa kizuizini" nchini Iran, familia yake imesema.

Robert Levinson, afisa mstaafu wa shirika la ujasusi la Marekani la FBI, mwaka 2007 kabla ya kutoweka kwake nchini nchini Iran (picha ya kumbukumbu).
Robert Levinson, afisa mstaafu wa shirika la ujasusi la Marekani la FBI, mwaka 2007 kabla ya kutoweka kwake nchini nchini Iran (picha ya kumbukumbu). © AFP
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Marekani Donald Trump hajathibitisha rasmi kifo chake, lakini amesema kuwa inawezekana kuwa amefariki dunia.

"Hawajatwambia kuhusiana na kifo chake, lakini watu wengi wanaamini kuwa taarifa hiyo ni sahihi," Donald Trump amesema, huku akiongeza kwamba ni "jambo la kusikitisha".

Amekiri kwamba taarifa hiyo "inatia huzuni". "Amekuwa mgonjwa kwa miaka miaka kadhaa," rais wa Marekani amebaini, huku akikiri kwamba alishindwa kumrudisha nchini Marekani.

"Hivi majuzi tumepokea habari kutoka kwa maafisa wa Marekani ambao walikuwa wasimamizi wake kwamba mume na baba wa watoto amefariki dunia akiwa kizuizini baada ya kuzuiliwa kwa miaka kadhaa na mamlaka nchini Irani," familia yake imesema katika taarifa.

Bila hata hivyo kutoa sababu au tarehe ya kifo cha yule ambaye mara nyingi alikuwa akionyeshwa kama mateka wa zamani zaidi katika historia ya Marekani, familia yake imebaini tu kwamba kifo chake kilitokea kabla ya janga la Covid- 19.