URUSI-CORONA-AFYA

Coronavirus: Visa vipya zaidi ya 10,500 vya maambukizi vyatangazwa Urusi

Magari maalumu yakinyunyuzia dawa dhidi ya virusi vya Corona katika mitaa ya jiji la Moscow.
Magari maalumu yakinyunyuzia dawa dhidi ya virusi vya Corona katika mitaa ya jiji la Moscow. Sergei Kiselyov/Moscow News Agency/REUTERS

Idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona imepindukia 263,000 nchini Urusi baada ya visa vipya 10,598 kuthibitishwa leo Ijumaa. Hali ambayo inaendelea kuzua hofu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Kituo cha kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 kimesema kuwa jumla ya watu 2,418 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo hatari baada ya vifo vipya 113 vilivyothibitishwa kutokea ndani ya saa 24, huku watu 58,226 wakipona ugonjwa huo.

Idadi ya vifo vilivyotokana na maambukizi ya virusi vya Corona duniani kote imepindukia watu 300,000, ambapo vingi vya vifo hivyo vimetokea Ulaya na Marekani, tangu kuzuka kwake huko China, mwishoni mwa mwaka uliopita.

Marekani ndio yenye visa vingi kwa kuwa na vifo 85,194, ikifuatiwa na Uingereza vifo 33,614, Italia vifo 31,368, Ufaransa vifo 27,425 na Uhispania yenye vifo 27,321.

Ulaya bara ambalo limeshambuliwa vikali na virusi, ambapo mataifa kama Italia, Uhispania na Ujerumani ni miongoni mwa mengine 10 ambayo yana idadi kubwa ya maambukizi na vifo. Ujerumani inatarajiwa kuanza kuchukua hatua za kulegeza masharti ya mipakani Jumamosi, wakati mataifa mengine kadhaa ya jirani yatarajaiwa kuichukua hatua kama hizo kuanzia Juni 15. Umoja wa Mataifa umesema janga la corona limesaabisha matatizo ya akili duniani kote.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani kwa Ulaya, Hans Kluge amesema kasi ya usambaaji wa virusi vya corona kwa Ulaya, inapungua, lakini ameongeza kuwa lazima mataifa yaendelea kuwa madhubuti katika kukabiliana na janga hilo.