URUSI-SIASA-USALAMA

Kura ya maoni yapigwa kubadilisha Katiba Urusi

Kituo cha kupigia kura huko Gigemez katika Jimbo la Moscow, Juni 25, 2020.
Kituo cha kupigia kura huko Gigemez katika Jimbo la Moscow, Juni 25, 2020. REUTERS/Evgenia Novozhenina

Urusi inafanya kura ya maoni ya kubadilisha Katiba ya nchi ili kumuwezesha Vladimir Putin asalie madarakani hadi mwaka 2036 na atekeleze itikadi zake za kihafidhina katika Katiba.

Matangazo ya kibiashara

Kura hiyo inapigwa wakati nchi ya Urusi inaendelea kukabiliwa na janga hatari la Corona.

Tarehe rasmi ya "mashauriano ya kitaifa" ni Julai 1, lakini mamlaka ilifungua vituo vya kupigia kura Juni 25 ili kuepusha mikusanyiko mikubwa ya watu, kwa sababu ya janga la Covid-19.

Ili kuanzisha hatua kadhaa za kijamii, kura sasa zitatekelezwa kwa zaidi ya siku tano kote Urusi, hata katika mikoa ambayo inapambana na Covid-19 hivi sasa.

"Bila Putin, hakuna Urusi. " Haya ni maoni ya mkuu wa wafanyakazi wa Kremlin, na inadhihirishwa na mamilioni ya Warusi ambao kwa miongo kadhaa wamemchagua tena Vladimir Putin kuendelea kuwepo madarakani kama Waziri mkuu au rais.

Imani hii inaweza kurudiwa Julai 1, baada ya kura ya maoni ya kitaifa ya kurekebisha katiba ya Urusi, ili kumwezesha Rais Putin kupata nafasi nyingine ya miaka sita tena.

Ingawa Rais Putin hajasema kuwa anataka kuchaguliwa tena, hajakataa hilo, na kusababisha wakosoaji kumshtaki kwa kutengeneza njia ya kukaa madarakani kwa maisha, au angalau hadi 2036.

Mchakato huo wa kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba ulipendekezwa na rais Vladmir Putin na awali ulipangiwa kufanyika Aprili 22 lakini kutokana na kuzuka kwa janga la virusi vya Corona ukaakhirishwa.

Putin ameshakaa madarakani kama rais na pia kama waziri mkuu katika kipindi cha miongo miwili iliyopita na ni kiongozi aliyetawala kwa kipindi kirefu zaidi nchini Urusi tangu Joseph Stalin aliyekuwa kiongozi wa Soviet.