JAPANI-MAFURIKO-USALAMA

Japan yaonya kutokea kwa mafuriko zaidi katika maeneo mbalimbali

Mafuriko kutokana na mvua kumbwa yalisababisha maporomoko ya udongo katika baadhi ya maeneo nchini Japan, kama hapa katika kijiji cha Minamiaso, katika mkoa wa Kumamoto, kusini mwa Japani.
Mafuriko kutokana na mvua kumbwa yalisababisha maporomoko ya udongo katika baadhi ya maeneo nchini Japan, kama hapa katika kijiji cha Minamiaso, katika mkoa wa Kumamoto, kusini mwa Japani. Mandatory credit REUTERS/Kyodo

Mamlaka nchini Japan zimetoa onyo la mafuriko na maporomoko ya ardhi  kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na ambazo zimesababisha vifo vya watu 54 kwenye tukio la hivi majuzi.

Matangazo ya kibiashara

Maafisa wanatoa wito kwa wakazi wa mikoa hiyo kuendelea kuwa makini kwani bado maji yanaendelea kuongezeka katika mito ya mikoa ya Gifu na Nagano.

Maeneo hayo yanashuhudia mvua ambayo haijawahi kunyesha kwa miongo kadhaa. Maafisa wa mamlaka hiyo wanasema madhara makubwa kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yanaweza kutokea.

Mvua kubwa zilianza kunyesha siku ya Jumamosi na uharibifu mkubwa umefanyika baada ya mito kadhaa kuvunja kingo zao kwenye maeneo ya mabonde.

Miji mingi imefunikwa kwa maji, hali inayofanya vigumu kuzifikia jamii zinazohitaji msaada.

Mito Tisa ilifurika katika maeneo zaidi ya 10. Maporomoko ya ardhi yalifukia nyumba na kuzuia barabara

Siku ya Jumamosi, watu 200,000 waliombwa kuondoka katika nyumba zao, kulingana na shirika la habari la Kyodo.

Watu wamekwama kwenye maeneo zaidi ya 10 mkoani humo. Maafisa wanasema wanafanya kazi ili kuwafikia, ikiwa pamoja na kutengeneza barabara za muda.

Wale walio kwenye makazi ya dharura wanasisitizwa kuosha mikono na kuweka umbali unaostahili kutoka mtu mmoja hadi mwengine kuepusha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Mwezi Oktoba mwaka jana, mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Hagibis yaliua watu 90.